Na MWANDISHI WETU
TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo itakuwa katika kibarua kigumu kingine cha kusaka pointi tatu muhimu watakapokutana na wababe wa soka Afrika, Morocco.
Stars inashuka dimbani kucheza na Morocco, katika mchezo wa pili wa Kundi E, Kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, saa 4:00 usiku.
Kikosi hicho chini ya Kocha Adel Amrouche, ilianza vizuri kampeni hizo, baada ya wikiendi iliyopita kuwafunga Niger bao 1-0, kwenye Uwanja Marrakech nchini Morocco, hivyo leo inahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili iweze kukaa kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.
Amrouche, alisema,anatarajia kupata upinzani mkubwa katika mchezo huo, lakini hana presha anachohitaji ni matokeo chanya tu.
“Mchezo huu ni muhimu sana kwetu,utakuwa mgumu mno, ila sisi tunaimani tutafanya vizuri licha ya Morocco si timu ndogo tutakuwa na upinzani sana.
“Ila kwenye mpira wa miguu lolote linaweza kutokea kwa sasa timu ilipofikia, hatuwezi kuwahofia wapinzani, kikubwa watu waje uwanjani kwa wingi ili kutoa sapoti kwa wachezaji,” alisema Amrouche.
Mchezo huo ni kufa au kupona kutokana na kila timu kuhitaji matokeo katika mechi hiyo ili iweze kujiweka mazingira bora kwenye kundi lao.
