Na Fred okoth, TANGA,
Wananchi Kata ya Segera, Kitogonji cha Mongo Wilaya ya Handeni Vijijini, wameitupia lawama Shirika la Umeme nchini, Tanesco, kwa kushindwa kuwapa umeme unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Baadhi ya kaya 50 katika kitongoji ya Michungwani ambazo hazijawekewa umeme mpaka sasa baada ya kukataa kutoa mchango wa shillingi elfu Hamsini, ambazo wamekuwa wakidaiwa kuchanga ili kuwekewa umeme huo.
Wakiongea na waandishi wa Morningstar Post waliowatembelea katika maeneo yao, mradi huo haukuzingatia ramani kwani kaya hizo hamsini zimejengwa zamani na wengi wao walianza kuomba umeme wa kawaida tangu mwaka 2011, lakini hawajapewa.
Kwa uchungu na masikitiko makubwa, Mzee Francis Lwambo (70), mkazi wa Kwedilenga kwa niaba ya wenzake alisema,
“Ulipokuja umeme wa REA kwenye kitongoji chetu waliruka kutuunganishia umeme kwenye nyumba zetu na kupeleka umeme kwingine kwa kuwa tulikataa kutoa mchango ya elfu hamsini….. Kibaya zaidi, kuna chuo cha Kiislam kiitwacho Madrasat Salaam kilichopo hapa Michungwani, wanatoa elimu ya dini lakini kuna kuwa na mazingira hatarishi kwa ajili ya kukosa nishati ya umeme ya kusukuma maji kutoka bondeni kwa matumizi ya kiibaada.”
Alisema kijijini hapo kuna vichaka hatari kwa usalama wa Watoto wanaosoma katika chuo hicho.
Aliongeza kuwa vichaka vimekuwa vikisababisha wezi kuiba mifugo mara kwa mara kutokana na kuwepo na giza mahali hapo.
Morning Star Post ilifunga safari hadi chuoni hapo kujionea mazingira na kutaka kupata maoni ya mkuu wa chuo hicho, Ustadh, Nassor Rajab.
“Ni kweli wanafunzi wangu ambao ni zaidi ya mia mbili wanapata shida kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme hasa wakati wa jioni na usiku. Sisi hapa tuliombwa mchango na kama tungetoa huenda tungepewa umeme kwa sababu wale waliotoa walipewa,” alisema.
“ Mbaya zaidi, hata Meneja wa Tanesco anataarifa hizo za mchango na hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya mhusika ambaye anajulikana. Naomba serikali yetu sikivu atuonee huruma ili tupate umeme kunusuru maslahi mapana ya wananchi hawa,” alishauri.
Wananchi hao waliopo katika Wilaya ya Handeni Vijijini, wanahudumiwa na Tanesco Wilaya ya Korogwe.
Morningstar Post ilizungumza na Meneja wa Taneco Wilaya Korogwe Mhandisi Peter Kanoti ofisini kwake, alisema
“Ni kweli wananchi wapo ndani ya mradi wa REA lakini kwa mujibu wa mchoro, watapata umeme katika awamu ya pili,” alifafanua.
Akijibu malalamiko ya wananchi kuombwa fedha kama mchango kwenye mradi huo, alikiri kufahamu taarifa hizi kutoka kwa wanakijiji, lakini aliwashauri kama kuna kuna mtu aliyewaomba fedha akirudi tena akamatwe na kufikishwa kituo cha polisi ahojiwe na kusema aliyemtuma kuchangisha watu fedha.
“Hilo swala la mtu kuomba wananchi fedha kama mchango kwenye mradi ni kweli lakini baada ya kufanya uchunguzi tulingundua kwamba sio mfanyakazi wa Tanseco,” alifafanua.
Morningstar Post inaendelea kuchunguza na kuzitafuta kampuni zinazofanya mradi huo kuzungumzia malalamiko hayo ambayo kwa mujibu wa sheria wananchi wanatakiwa kulipa sh27000 ya kuunganishiwa umeme na sio sh50,000.
Wanafunzi wa Chuo cha Kiislam Michungwani Tanga, wanaosoma nje ya madarasa nyakati za jioni kwa kukukosa umeme licha ya umeme kufika na kupita kutoka kijiji hicho na kufungwa vijiji vya jirani