Na MWANDISHI WETU

BAADA ya kupewa mikoba ya kukinoa kikosi cha Coastal Union ya Tanga, Kocha wa mpya wa klabu hiyo, David Ouma ameahidi kuirudisha timu hiyo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC) msimu huu.

Ouma amejiunga na klabu hiyo akichukua mikoba ya Mwinyi Zahera, na akasaini mkataba wa miaka miwili akitokea kwao Kenya alipokuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa hilo ‘Harambee Stars’.

Akizungumza siku chache tu baada ya kusaini mkataba na timu hiyo, Ouma amesema kinachompa matumaini ni ubora wa wachezaji wengi wa timu hiyo pamoja na vipaji walivyonavyo.

“Nimevutiwa na vitu vingi kwa muda mfupi tangu nimejiunga na Coastal, kikubwa ni uwezo wa wachezaji, wengi wana umri mdogo na ni wapambanaji naamini nikiongeza mbinu zangu tutakuwa miongoni mwa timu zinazopigania ubingwa msimu huu,” amesema Ouma.

Pia, amesema anajua hawapo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, lakini malengo yake ni kutumia mapumziko ya kalenda ya FIFA, kukiimarisha kikosi hicho ili ligi itakapoendelea waweze kupata matokeo mazuri.

Amesema baada ya kutambua uwezo wa wachezaji atakachokifanya ni kukabidhi majukumu kwa kila mchezaji ili kuhakikisha wanatimiza malengo ambayo wamekusudia kuyafikia msimu huu.

Coastal Union ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo, ikiwa na pointi saba tu, katika michezo tisa iliyocheza, huku ikishinda mchezo mmoja, imefungwa minne na kutoka sare mechi nne

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *