Na MWANDISHI

ZIKISALIA siku tisa tu kabla ya Yanga kucheza mechi ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, ameuomba uongozi wa klabu hiyo kumtafutia mechi ya kirafiki ili kukipima kikosi chake.

Yanga itatupa karata yake ya kwanza hatua hiyo ya makundi kwa kukung’utana na CR Belouizdad ya Algeria, Novemba 24, mwaka huu, utakaopigwa Uwanja wa 5 July 1962, jijini Algers.

Katika kundi hilo D, Yanga imepangwa na CR Belouizdad, Medeama ya Ghana na Al Ahly ya Misri.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Kocha Gamondi amesema anahitaji mchezo wa kirafiki kabla ya kuvaana na Belouizdad ili kukiweka sawa kikosi chake.

“Tumepata mapumziko kutokana na ligi kusimama kwa mechi za timu za taifa, tunafanya sana mazoezi kuhakikisha tunakuwa bora katika mchezo ujao, tunahitaji mchezo wa kujipima nguvu.

“Nimezungumza na viongozi watafute timu ambayo itatupa ushindani tucheze nao Jumamosi, baada ya mchezo huo ndiyo tutafanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo mkubwa,” amesema.

Kocha huyo kutoka Argentina amesema tayari ameanza kuifuatilia CR Belouizdad na kubaini ubora na udhaifu wao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *