Na Mwandishi wetu
BAADA ya kuichapa Simba mabao 5-1 jana, Kipa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC), Yanga, Djigui Diarra amesema kwa sasa hakuna walichobakisha ili kuthibitisha ubora wao.
Simba jana ilipokea kipigo hicho cha aibu kutoka kwa Yanga, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Maneno hayo ya Diarra aliyasema kupitia ukurasa wake wa Instagram akijimbwafai kwa kusema kwa sasa wao ni bora, hawana shida tena ya kujitambulisha katika ardhi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Diarra ameandika hivi; “1,2,3,4,5, kweli hakuna tulichobakisha kuthibitisha ubora wetu waungwana, hiki ni kiwango cha juu sana, this is MASTARCLASS.”
Kwa ushindi huo Yanga imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 21, ikifuatiwa na Azam FC wenye alama 19, huku Simba yenye pointi 18 wakishika nafasi ya tatu.
