Na Mwandishi Wetu
Mapinduzi ya kisiasa kwa kawaida ni matumizi ya nguvu yanayojaribu kuhusisha watu kusitisha utawala wa serikali iliyoko madarakani na kusimamisha serikali nyingine.
Mapinduzi ni mabadiliko ya haraka upande wa siasa na miundo yanayotokana na shinikizo la wananchi, linalotumia mara nyingi nguvu kuiondoa serikali yoyote madarakani.
Katika historia ya binadamu mapinduzi yalitokea mara nyingi kwa sababu, mbinu, muda na malengo mbalimbali.Hayo yalifuatwa na athari kubwa juu ya utamaduni na uchumi wa jamii husika.
Pengine mabadiliko hayo ya mwisho pia yanaitwa mapinduzi hata yasiposababisha serikali ianguke.
Lakini mapinduzi haya yanayozungumzwa hivi sasa hapa nchini ni mapinduzi yatakayohusisha nguvu ya umma kushiriki kwa kuiondoa serikali ya Chama cha Mapinduzi CCM inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan.
Tamko la Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP, Camillus Wambura, kuwaonya watu wanataka kuhamasisha wananchi kuandamana kwa lengo la kuiangusha serikali iliyoko madarakani haiwezi kukubalika kwa watanzania.
Licha ya IGP Wambura kuwataka watanzania kutokusikiliza watu hao na kuwapuuza, watanzania hawawezi kukubali upuuzi wa watu wachache kutaka kufanya mapinduzi yasio ya kidemokrasia.
Watanzania wanaamini kuwa serikila ya CCM iliyoko madarakani waliichagua kwa kupiga kura na kuiweka madarakani wanaamini kuiondoa madarakani ni kwa njia ya kidemokrasia na sio vinginevyo.
Aidha, sera za kimataifa duniani na Umoja wa Nchi za Afrika hautaki kuona serikali zinaongoza nchi kwa mapinduzi ya kisiasa bila kuhusisha taratibu za kidemokrasia ambazo zinahusisha matakwa ya wananchi.
Vikundi vya watu wanaochochea harakati hizi za kutaka kuipindua serikali ya CCM, ni wanasiasa wa maji taka ambao wanaendesha siasa zisizofaa, wasio kuwa na sera, urafi wa madaraka na hawana uwezo wa kuongoza nchi hii.
Kikundi hicho ambacho kinatangaza kuhamasisha wananchi kuiangusha serikali iliyoko madarakani, wanatumia hoja na vigezo dhaifu sana zikiwemo hoja za uwekezaji wa kibiashara kwenye bandari.
Hajo kama hizi haziwezi kukubalika kuwafanya watanzania kushawishika kuingia katika harakati za kuipindua serikali ya CCM kwa njia zisizokuwa za kidemokrasia.
Jeshi la Polisi limekuwa imara kwa kuliona hili na kulikemea mapema kabisa na kufanya kazi kwa weledi mkubwa wa kuzuia makosa badala ya kusubiri mambo yaharibike ndio waanze kuchukua hatua, hapo tunalipongeza jeshi letu kwa weledi huu.
Wanaotaka kuleta uchochezi huu wa kuhamasisha watu kupindua serikali yao ni watu waliokuwa hawana sera na wenye urafi wa madaraka kwa manufaa yao binafasi.
Ni watu ambao wameshindwa kutangaza sera za kisiasa wakaeleweka kwa wananchi ili kuweza kukubalika na kuingia madarakani kwa njia ya kidemokrasia na sio kwa vurugu na nguvu ya umma.
Jambo hili kwa hapa nchini kwetu haliwezi kukubalika hata kidogo kwa kuwa watanzania tuliachiwa misingi mizuri na mwalimu Nyerere ya heshima, nidhamu na uti wa sheria za nchi na uzalendo wa kweli kwa nchi yetu.
Watanzania wameendelea kufuata misingi hii ya kwa awamu zote za maraisi waliotangulia ambao wamekuwa wakipokezania vijiti katika kuongoza serikali kwa amani kabisa.
Tunawataka viongozi wa jeshi la polisi kuchukua hatua kwa watu hao wanaoanza chokochoko mapema na kukomesha kabisa michakato ya aina yoyote yenye sura ya kuleta uchochezi na kuvunja sheria za nchi, mapinduzi ya serikali ya CCM inayongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan hayawezi kukubalika hapa nchini.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP, Camillus Wambura