Na Mwandishi Wetu

Baadhi ya vifaa vilivyoko katika kituo cha kufua umeme cha IPTL vimeendelea kuibiwa, licha ya kuwa kuna ulinzi mkali.

Kituo hicho kilichopo Tegete jijini Dar es Salaam, vifaa vyake mbalimbali kama waya za copper na mafuta ya transfoma vinaendelea kuibiwa na kuacha kituo hicho kikiwa gofu.

Uchunguzi uliofanywa na Morningstar Post umebaini kuwa Juni 28, mwaka huu vifaa hivyo viliibiwa na kuuzwa kwa mfanyabiashara mmoja aliyefahamika kwa jina la Makolo aliyeko maeneo ya Tegeta ambaye simu anayotumia imesajiliwa kwa jina la Winfrida Simon.

Inadaiwa vifaa hivyo baada ya kuuzwa kwa mfanyabishara huyo vilipelekwa kuuzwa katika kiwanda cha kuyeyusha vyuma Temeke.

Akizungumza na Morningstar POST Bw. Makolo alikataa kujibu lolote akitaka kutajiwa namba ya gari iliyompelekea mzingo huo wa wizi.

“Wewe sio mwandishi wa habari kama kweli wewe ni mwandishi wa habari umesema nililetewa vitu vya wizi uniambie gari hiyo ilikuwa namba gani ili ukweli uweze kujulikana, lazima ijulikane” alisema Makolo.

Habari zinadai kuwa walinzi wa kituo hicho walihusika kwa kushirikiana na wezi kuiba vifaa hivyo.

Matukio ya kuibiwa vifaa vya IPTL yamekuwa ni mwendelezo kwani huko nyuma viliibiwa na kuripotiwa kituo cha polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam.

Hata hivyo juhudi za kumpata Kamanda Maalumu ya Dar es Salaam ACP Jumanne Mlilo, hazikuweza kufanikiwa mara moja lakini tunaendelea kumtafuta kuzungumzia tukio hilo.

0744499499

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *