Kanisa la Moravian Dar Watifuana

*Mfadhili ahusishwa kuwagawa waumini*

Kanisa la Moravian Usharika wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, hali sio shwari baada ya  kuibuka mvutano mkubwa kati ya viongozi na waumini.

Hali ndani ya kanisa hilo imechafuka baada kuibuka mvutano mkubwa na baadhi ya waumini kuwekwa mahabusu kwa madai ya kufanya fujo kanisani.

Waumini wa kanisa hilo Emmy Joram, Mess Mwakafambo na Jacob, walikamatwa na polisi Kanda Maalum jijini Dar es Salaam Machi 11 mwaka huu, kwa madai ya kufanya fujo kanisani.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Mlilo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo hakuweza kutoa taarifa zaidi kwa kuwa hakuwa na taarifa hizo, lakini aliahidi kufuatilia na kutoa maelezo badae.

Hata hivyo habari kutoka ndani ya kanisa hilo, kwa baadhi ya waumini ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema kuwa kumekuwa na hali ya unyanyasaji na uonevu ndani ya kanisa hilo kwa baadhi ya viongozi na mfadhili wa kanisa hilo kutumia madaraka yao na uwezo wao wa fedha kunyanyasa waumini.

Walisema kuwa hali ndani ya kanisa hilo sio shwari kwa kuwa kuna mvutano mkali na kutokuelewana kati ya viongozi, waumini na mfadhili wa kanisa hilo ambaye ni Wakili wa Mali za Kanisa hilo, Bw. Yona Sonelo.

Wakizungumzia tukio la kukamatwa kwa waumini wa kanisa hilo, mwezi Machi mwaka huu kwenye misa iliyofanyika kanisani kwao, baadhi ya waumini walionesha hisia zao kwa kuonesha mabango ndani ya kanisa kulenga mambo yanayofanywa na viongozi na mfadhili wao.

Walisema kuwa mabango yalishikiriwa na baadhi ya waumini yalikuwa yanasomeka kama vile Sonela anatutesa, bango lingine lilisomeka Hatutaki viongozi wetu waachishwe tunawapenda, bango lingine lisomeka Mchungaji usiwasikilize matajiri tusikilize na sisi maskini.

“Baada ya waumini kuonesha mabango hayo cha kushangaza siku ya tatu walipigiwa simu na polisi kituo cha kati na kuhojiwa na kuswekwa lupango wakaambiwa wamefanya fujo kanisani”, alisema mmoja wa waumini hao.

Alisema baada ya kuwekwa ndani walitolewa dhamana na viongozi wa kanisa kutoka jimboni na kuambiwa waendelee kuripoti polisi na mpaka sasa wanaendelea kuripoti.

Waumini hao wanahoji, je ni nani aliyekuwa mlalamikaji katika kesi hiyo, kama ni viongozi wa kanisa kwa nini walikwenda kuwawekea dhamana, je kama ni mfadhili wa kanisa kwa nini hajajitokeza mpaka sasa.

Mfadhili wa kanisa hilo ambaye pia ni Wakili wa Mali za Kanisa Bw Yona Sonela, alipoulizwa na Morningstar Post kuhusu suala hilo la waumini kuwekwa polisi, hakutaka kuzungumza lolote.

“Nani kakutuma….wewe si una’chombo cha habari andika hizo taarifa” alisema Bw Sonela na kukata simu.

Wakimzungumzia mfadhili huyo, waumini hao walisema kuwa wana uzoefu nae hata alipokuwa kwenye usharika wa kanisa hilo Tabata, alikuwa akitofautiana na waumini kutokana na kauli zake akitoa msaada kwa majigambo.

Walisema kuwa mbali na misaada mikubwa anayotoa, aliwahi kujenga madhabahu kwenye usharika wa Tabata, na kuleta majigambo ikapelekea waumini kuvunja madhabahu hiyo na kujenga upya kwa nguvu zao wenyewe hatua ambayo ilipelekea mfadhili huyo kuhama usharika na kurudi kwenye usharika wake wa zamani wa Uhuru.

“Ni kweli Mungu kamjalia fedha anatusaidia lakini msaada yake ina unyanyasaji…amefadhili kununua vyombo vya kwaya vyenye thamani ya mamilioni vinaweza kuwa ni vifaa bora na vyenye thamani kuliko vifaa vyote kwenye makanisa yote mengine”, alisema mmoja wa waumini hao.

Alisema kuwa amekuwa akifadhili nguo za sare za kwaya amefadhili kuleta kwaya ya Joyous Celebration kutoka Afrika Kusini Septemba 9, mwaka jana na kutumia mamilioni ya fedha, lakini amekuwa akitumia fedha kuwagawa waumini wa kanisa hilo.

Hata hivyo mchungaji wa kanisa hilo Abraham Mwangosi alipoulizwa na Morningstar Post hakutaka kuzungumza lolote kwa kuwa yeye sio msemaji wa kanisa.

0744 499499

Askofu Jimbo la Mashariki Kanisa la Moravian, Mchungaji Lawi Mwankuga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *