Viongozi wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki, wamekuja juu wakitaka taasisi hiyo isihusishwe na mabishano ya mkristo mmoja na mwenzake kama ni ya kanisa zima.
Msemaji Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki, Gerhard Sikali, alikanusha habari iliyorushwa na tovuti hii yenye kichwa cha habari Kanisa la Morovian Dar Watifuana, *mfadhili ahusishwa kuwagawa waumini*.
Akijibu habari hiyo kwa njia ya barua pepe, Sikali alisema kuwa aliyetoa taarifa hiyo kwenye chombo hiki cha habari hana nia njema kwa taasisi yao.
“Aliyetoa habari hii hana nia njema na taasisi hii, maana siye msemaji wa kanisa au taasisi hii. Ni kosa la kumkosea baba Askofu wetu kurusha picha yake kwa kutilia mkazo habari hiyo bila kibali chake,” alisema Sikali.
Akasisitiza kuwa kanisa hilo kwa ujumla liko shwari na mshikamano mzuri na mabishano ya mkristo mmoja na mwezake yasijumuishwe kana kwamba ni kanisa zima.
Licha ya uongozi wa kanisa hilo kutupia lawama Morningstar POST, kuandika habari hiyo kwa kuhusisha kanisa, uongozi wa kanisa bado unashindwa kutolea ufafanuzi mgogoro uliopo baina ya mkristo mmoja na mwenzake wanaosema kuwa ndio wenye mgogoro na sio kanisa.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na Morningstar POST na kuhusisha kanisa kuwa liko katika hali isiyokuwa shwari baada baadhi ya waumini wa Usharika wa Uhuru Dar es Salaam kufikishwa polisi na kuswekwa mahabusu, uongozi wa kanisa hilo bado uko katika kigugumizi kuzungumzia suala hilo.
Kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo, pindi kunapotokea kutokuelewa kwa viongozi au waumini masuala hayo hushughulikiwa na kanisa na inapobidi kupelekwa polisi mwenye mamlaka ya kutoa ruhusa suala hilo lipelekwe polisi ni katibu wa jimbo.
Katika taarifa inayolalamikiwa na viongozi hao kuwa haikutolewa na msemaji wa kanisa, baadhi ya waumini wa kanisa hilo ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walisema kuwa viongozi na mfadhili wa kanisa hilo wanatumia nafasi zao na uwezo wa kifedha kunyanyasa waumini.
Hatua ambayo ilipelekea wakati wa misa kanisani waumini kuonesha bango yanaeleza hisia zao jambo lililosababisha kuitwa polisi na kuswekwa mahabusu na mpaka sana wanaendelea kuripoti polisi na haijajulikana aliyewashtaki polisi ni nani, licha ya viongozi wa jimbo kuwawekea dhamana.
0744 499 499

Askofu Jimbo la Mashariki Kanisa la Moravian, Mchungaji Lawi Mwankuga