Kampuni ya Haomai Investment Co. Ltd ya jijini Dar es Salaam, inayoendeshwa na raia kutoka China, imetiliwa mashaka na kufanyiwa ukaguzi wa uzalishaji wake wa mabati hapa nchini.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kampuni hiyo, ambayo pia inazailisha mitambo ya kuchanganya kokoto, maafisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walifika kufanya ukaguzi wa mabati yanayozalishwa na kampuni hiyo wiki iliyopita baada ya kuyatilia mashaka.
Hata hivyo, hatua hiyo ya TBS kufika kufanya ukaguzi ni baada ya kuwepo taarifa kuwa kampuni hiyo inazalisha mabati tofauti na viwango vinavyotakiwa na sheria ya viwango nchini.
Mtoa taarifa alisema kuwa TBS walifika na kutilia mashaka ubora wa viwango vya mabati hayo na kuchukua sampuli kwa ukaguzi zaidi.
Akizungumza na Morningstar Post, kwa niaba ya uongozi wa kampani hiyo, mshauri wa kampuni hiyo alijitambulisha kwa jina moja la Haule, alikiri kuwa TBS walifika na huwa wanakagua mabati ya kiwanda hicho mara kwa mara.
“TBS wamekuwa wakikagua mabati kila mara yanapokuwa yanaingia hapa nchini….taarifa za kuwa tunazalisha mabati yasiokuwa na viwango sio za kweli….na wenyewe (wachina), hawataki waandishi kufanya uchunguzi wowote,” alisema Haule.
Awali kiongozi wa kampuni hiyo raia wa China ambaye hakutaka kujitambulisha alikiri kuwa TBS walifika kukagua na wanasubiri majibu kutoka TBS.
Aliongeza kuwa wanazalisha mabati ya viwango vinazotakiwa isipokuwa kwa yale mabati yanayohitajika kwa ajili ya kujengea uzio na mabanda ya mifugo wanazalisha kwa viwango tofauti na vinavyotakiwa na sheria.
Hata hivyo kiongozi mwingine raia wa China aliyejitambulisha kwa jina la Fred, alisema kuwa TBS wanakagua mabati yao kila mara na kuhusu ubora yameshathibitishwa.
“Hata leo tumetoka TBS kufutilia masuala haya….hakuna tatizo kwa taarifa zaidi wasiliana na msemaji wetu Haule” alisema Fred.
Awali Morningstar Post alipata taarifa kuwa maafisa wa TBS walifika kiwandani hapo wiki iliyopita baada ya kutilia mashaka mabati yanayozalishwa na kiwanda hiyo kuwa ni viwango vya chini vya geji 36 tofauti na viwango vinavvyotakiwa.
Juhudi za kuwapata viongozi wa TBS kuzungumzia suala hilo hazikuweza kufanikiwa mara moja. Hata hivyo juhudi za kuwatafuta kuweza kutoa taarifa rasmi zinaendelea.
