NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Huaxia New Energy Technology inadaiwa kukiuka sheria na taratibu mbalimbali za nchi kwenye ujenzi unaoendelea wa kiwanda kinachojengwa Pangani, Kibaha, Mkoani Pwani.
Uchunguzi uliofanywa na MorningStarPost, umebaini kuwa miongoni mwa mambo ambayo wanakiuka wamiliki wa kampuni hiyo kutoka China, ni kufanya ujenzi kwa kutumia vibao vya kampuni nyingine ambazo wafanyakazi wake na wataalamu hawapo kwenye eneo la mradi kwa lengo la kupunguza matumizi ya fedha.
Chanzo kilichopo kwenye eneo hilo la ujenzi wa kiwanda ambacho kinaelezwa kitajihusisha na masuala ya umeme jua, kimedai kwamba kampuni hiyo imechukua mafundi wa kawaida ndio wanaojenga kiwanda hicho.

Mhandisi Juma Mhando, aliyezungumza na mwandishi wetu kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa wakati wa kuweka bango la ujenzi, ni kwamba, kila kampuni ambayo imeandikwa kwenye ubao wa mradi, inapaswa mafundi na wataalamu wake wawe kwenye eneo husika, lakini hivisasa hilo halifanyiki.
“Siku hizi watu wanafanya biashara ya kuuza vile vibao tu, mtu anataka kujenga, anailipa kampuni za ujenzi, wakishamalizana wao wanaendelea na ujenzi bila mafundi wa kampuni husika kuwepo kwenye eneo la mradi, hili linabidi likomeshwe,” alisema Mhandisi Mhando.
Aidha, uchunguzi zaidi umebaini kuwa, mafundi wanaoshiriki kwenye ujenzi wa mradi huo, hawana mikataba; wanalipwa kwa siku na hivyo iwapo watapata ajali wakiwa kwenye eneo la kazi, hawatahudumiwa.
“Hapa hakuna mwenye mkataba, kama itatokea mtu ameumia akiwa kazini na hizi kazi za ujenzi ajali ni kitu cha kawaida,” alisema mmoja wa mafundi alipozungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Alisema, wamezoea kuona sehemu nyingine wanatembelewa na maafisa wa kukagua usalama wakiwa kazini, lakini tangu wameanza ujenzi huo, hawajaona hilo likifanyika, ndio maana wenye kampuni hiyo hawajali usalama wa wafanyakazi wao.

Jambo jingine ambao uchunguzi wa MorningStarPost umebaini, wapo raia wa China ambao wanafanyakazi ambazo zilipaswa kufanywa na Watanzania, na inadaiwa wanalipwa mshahara mkubwa, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya kulinda ajira za wazawa.
“Kuna kazi kama kuendesha Toyo, hiyo wamepewa Wachina wakati Watanzania wazawa walikuwa na uwezo wa kuifanya, lakini wamepeana wenyewe na wanalipana mishahara mikubwa sisi tunaminywa tu,” kilisema chanzo chetu, huku kikisisitiza yapo mambo mengi ambayo yanaendelea na iwapo Serikali kwa kutumia mamlaka zake mbalimbali ikifika kwenye eneo la mradi itayabaini.
Wakizungumza na waandishi wetu, wamiliki wa kampuni hiyo kwa msaada wa Mkalimani wao aliyejulikana kwa jina moja la David, walikiri kuwepo kwa mapungufu hayo.
Hata hivyo, waandishi wetu wanaendelea kufuatilia taarifa nyingine ambazo zimepatikana na umma utajulishwa ili hatua zichukuliwe.