Na OWM – TAMISEMI
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OWM-TAMISEMI ) Bw. Adolf Ndunguru amewataka wataalamu wa TEHAMA katika ngazi ya Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha wanasimamia mifumo ya kidigitali kwa weledi, usalama na ufanisi ili kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi nchini.
Akifungua kikao kazi cha wataalamu wa TEHAMA wa Sekretarieti za Mikoa Jijini Dodoma amesema Serikali imeendelea kutambua nafasi kubwa ya TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za umma, hivyo wataalamu wa sekta hiyo wanapaswa kuhakikisha mifumo yote ya kidigitali inafanya kazi kwa tija inayotarajiwa katika ngazi za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amefafanua kuwa dunia inaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kidigitali yanayochochea matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utawala, uchumi, utoaji wa huduma na maendeleo ya jamii kwa ujumla, hali inayolazimu wataalamu wa ndani ya Serikali kwenda sambamba na mabadiliko hayo.
“Ni wajibu wa wataalamu wa TEHAMA kuhakikisha mifumo ya kidigitali inalindwa na kusimamiwa kwa viwango vya juu vya usalama na ufanisi ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa wakati,” amesema Bw. Ndunguru
Aidha, amewataka wataalamu hao kuibua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao kwa kutumia TEHAMA ili kuongeza tija katika shughuli za maendeleo na uchumi wa wananchi.