Na Shaban Juma, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Mheshimiwa. Dkt. Florence Samizi amesema Tanzania imeendelea na hatua za kuzuia na kuimarisha utayari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo unaoendelea katika nchi za Jamhuri ya Demokrasia Kongo na Uganda, huku akisisitiza mshikamano wa kikanda na umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kulinda usalama wa afya wa wananchi.
Dkt. Samizi amesema hayo Mei 26, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa mjadala kuhusu mlipuko wa Ebola katika nchi hizo, ulioandaliwa jijini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, ambapo ameshiriki kwa njia ya mtandao akiwa katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Katika mjadala huo, Tanzania imeeleza mshikamano wake na Serikali pamoja na wananchi wa DRC na Uganda kufuatia mlipuko huo, huku ikitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele wakitoa huduma.
Aidha Dkt. Samizi amesema Tanzania inatambua uratibu wa shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Maambukizi cha Afrika (Africa CDC) na itaendelea kushirikiana na kutekeleza hatua za pamoja katika kushughulikia masuala ya dharura ili kuendelea kulinda afya za wananchi