Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewahakikishia wakazi wa Kimanzichana mkoani Pwani kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye lengo la kuinua uchumi na kuwahimiza wananchi kuunga mkono juhudi hizo ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya kilometa 43.83 kutoka Kimanzichana kupitia Mkamba hadi Msanga, Ulega amesema kuwa Serikali tayari imeshatoa fedha zinazohitajika na kwamba maandalizi ya utekelezaji yako katika hatua za mwisho.
“Ndugu wananchi, nawahakikishia kuwa Serikali yenu chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mnakuwa na mazingira bora ya kufanya shughuli zenu za maendeleo. Uthibitisho wa hilo ni pamoja na kutolewa kwa zaidi ya shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya mradi huu,” alisisitiza Ulega.
Waziri huyo aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni mara baada ya msimu wa masika kumalizika. Pia aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kusimamia kwa karibu mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.
Aidha, Ulega alielekeza Meneja wa mradi kutoa kipaumbele cha ajira za muda kwa wakazi wa eneo hilo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wao, wakazi wa Kimanzichana walioshiriki mkutano wa hadhara walieleza shukrani zao kwa serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za mradi huo. Wamesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hasa mazao ya kilimo na biashara ndogondogo, hivyo kuboresha maisha yao kwa ujumla.