LICHA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kupitia kwa Katibu wake na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Sylvester Yaredi kupiga marufuku vitendo vya ukiukaji wa kanuni na maadili ya chama hicho, vitendo hivyo vinadaiwa kushamiri kwenye Kata ya Buyuni, Wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Kupitia waraka wake alioutoa kwenda kwa wabunge na madiwani ambao mwandishi wa habari hizi amepata nakala yake, Yaredi amewataka wagombea pamoja na mambo mengine, wajiepushe na vitendo vya rushwa, huku akipiga marufuku kampeni chafu za kuharibu sifa za wagombea wengine.

Hata hivyo, licha ya makatazo hayo, baadhi ya wapambe wa diwani aliyemaliza muda wake Athumani Maembe Ally, wanalalamikiwa kusambaza ujumbe mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwachafua wagombea wengine akiwemo Jesca Motto, ambaye anagombea nafasi ya udiwani.

Wapambe hao wa Maembe akiwemo aliyetajwa kwa jina la Halima Mkambula, ambaye alikuwa mmoja wa watiania wa udiwani wa Viti Maalum Ilala, kwenye moja ya taarifa zake alizosambaza kwenye mitandao ya kijamii (mwandishi ameziona) anakiri kwamba anampigania mgombea huyo (Maembe) kwasababu ni baba yake wa kumlea, huku akiwachafua wagombea wengine kwa tuhuma nzito ambazo hatuwezi kuziandika kwasababu za kimaadili.

Ingawa, kupitia ujumbe huo hakutaja jina la mlengwa, lakini tuhuma hizo zinaonekana kumlenga moja kwa moja Jesca Motto, ambaye ni mwanamke pekee aliyejitokeza kugombea udiwani kwenye Kata hiyo inayokua kwa kasi, huku ikidaiwa wapambe hao wanafanya hivyo kwa kile kinachodaiwa ni hofu ya nguvu kubwa aliyonayo (Jesca) ambaye anatajwa kukubalika ndani na nje ya chama hicho tawala.

Wanachama mbalimbali wa CCM kata ya Buyuni tangu zilipoanza kampeni chafu dhidi ya mgombea huyo, wamelaani vikali vitendo hivyo, huku wakishangazwa na kitendo cha Maembe kunyamazia vurugu za wapambe wake, huku wakiomba chama kichukue hatua ili kujenga nidhamu wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.

“Kinachoendelea hapa kwenye Kata yetu ni udhalilishaji, huyu mgombea anazushiwa mambo mengi sana ili ionekane hafai wakati viongozi wa chama Taifa wamempitisha kuwa mgombea na hii sio mara yake ya kwanza, mara zote amekuwa akishika nafasi ya pili kwenye kura za maoni, ninachokiona hapa ni hofu, kama mtu anajiamini na anajisifia amefanya mambo makubwa kwenye kata yetu, kwanini awatume wapambe wake wawachafue wagombea wengine?,” alihoji mmoja wa wanachama wa CCM ambaye hakupenda jina lake litoke hadharani.

Mwanachama huyo alisema, kitendo kinachofanywa na wapambe hao, hakikubaliki, kwani mbali na kumchafua mgombea huyo ambaye amepitishwa na vikao vya vya juu vya CCM, wanakichafua chama na kuwachafua waliompitisha.

“Unatoa tuhuma mbaya kama zile ambazo hazina maadili, huku ukijua ni uongo kwa lengo la kumdhalilisha mgombea mwingine ili wako aonekane bora, ni jambo baya sana, tena unamzushia mgombea ambaye amepitishwa na chama, hii maana yake unakichafua chama, ni utovu wa nidhamu,” alisisitiza mwanachama huyo kwa hisia.

Wanachama wengine wengine waliozungumza na mwandishi wetu, waliomba uongozi wa CCM Wilaya ya Ilala na Mkoa kutupia jicho kinachoendelea kwenye kata hiyo.

Walisema, kwenye kata yao kuna ukiukwaji mkubwa wa kanuni na maadili ya chama ikiwemo matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kuwashawishi wajumbe wapitishe wagombea fulani kwenye mkutano unaotarajia kufanyika kesho, Agosti 4, 2025 kwenye Kata ya Buyuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *