NA MWANDISHI WETU

WANACHAMA wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara, ambao iliripotiwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii, wamemuomba radhi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya na mgombea udiwani wa Kata ya Mangaka, Salvatory Lyimo.

Miezi kadhaa iliyopita, Morningstarpost iliandika habari kuhusu makada hao akiwemo Shaibu Milanzi (pichani) ambaye ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Mhata, kupitia kundi la mtandao wa kijamii la mbunge huyo, wanadaiwa kumkashifu Lyimo.

Wanachama hao wanadaiwa kutoa tuhuma (ambazo hatuwezi kuziweka hadharani kwasababu za kimaadili) zenye lengo la kumdhalilisha na kumvunjia heshima Lyimo kwa jamii ya jimbo hilo, huku ikidaiwa chanzo ni sababu za kisiasa.

Mbali na tuhuma hizo dhidi ya Lyimo, kwa muda mrefu kikundi hicho cha watu ambao wanatajwa kuwa ni wapambe wa Mbunge wa Nanyumbu, wamekuwa wakimbagua Lyimo kwasababu anatoka Kanda ya Kaskazini.

Inaelezwa, wamekuwa wakimtolea maneno ya kibaguzi na kumtaka akagombee kwao kwa maana ya Mkoa wa Kilimanjaro, jambo ambalo limekuwa likimuhuzunisha, kwani vitendo hivyo ni kinyume na Katiba ya nchi ambayo inamruhusu Mtanzania yeyote kwenda kuishi popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kugombea nafasi yoyote ambayo ataona inaendana na sifa alizonazo.

Kwa mujibu wa barua ambayo mwandishi wa habari hizi ameiona, iliyoandikwa na Milanzi kwenda kwa Lyimo, amekiri kumchafua mwanachama mwenzake huyo kupitia mtandao wa kijamii kwa kuweka machapisho yasiyo na staha.

“Kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria (defamation), naomba kupitia barua hii kukuomba msamaha kwa kitendo hicho, na kwamba jambo hilo halitajirudia tena aidha kwenye halaiki au mitandao ya simu,” aliandika Milanzi.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa, wapambe hao wa mbunge anayemaliza muda wake walimshambulia Salvatory Lyimo kwa lengo la kumdhoofisha kutokana na nguvu yake kisiasa, huku wakilenga kutaka kupanga safu ya uongozi kwenye nafasi ya udiwani kwenye kata mbalimbali za Jimbo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *