NA MWANDISHI WETU

Jeshi la Polisi Kanda Maalum, Dar es Salaam, Tanzania, limesema linawashikilia watu 8 kwa tuhuma za tukio la kujaribu kuteka la Novemba 11, 2024, katika mkoa huo.

Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi, Muliro J. Muliro – amesema watuhumiwa wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika Mikoa ya Dar es Salaam, Songea, Ruvuma na Morogoro, pia wamekamata gari aina ya Toyota Raum waliyoitumia wakati wa tukio ikiwa na namba T 237 EGE ambayo si halisi, na uchunguzi umebaini namba halisi ni T237 ECF.

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Bato Bahati Tweve 32, Yusuph Abdallah 32, Fredrick Juma 31, Nelson Elimusa Msela 24, Benk Daniel Mwakalebela 40, Thomas Ephraim Mwakagile (45), Anitha Alfred Temba 27 na Isack Mwaifani Bondia.

Novemba 11 video ilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii, ikionyesha watu kadhaa wakijaribu kumuingiza kwenye gari kwa nguvu mfanyabiashara, Deogratius Tarimo, Mkazi wa Kibaha.

Tangazo la polisi linakuja siku chache tangu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo kutangazwa kutekwa kabla ya kuachiliwa akiwa na majera katika jiji la Dar es Salaam

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *