Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan

NA MWANDISHI WETU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema matukio ya mauaji yanatokea katika kila nchi na Tanzania haijawahi kuagiza Balozi wake aseme jambo kwa nchi nyingine.

“Utasikia mtoto kabeba bunduki kaenda kushambulia shule, kadhaa wamekufa, kufa kupo tu. Kwa njia yoyote matukio haya yanatokea katika kila nchi.”

Ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya kufunga Mkutano wa Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo, yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Rais Samia amesema matukio haya yanapotokea katika nchi nyingine, “sisi hatujawahi kuziambia nchi kupitia balozi wetu, ‘hebu waambie hao.’ Sasa wengine wasiwe mafundi wa kutuelekeza nini cha kufanya.”

Kauli ya Rais Samia imekuja wiki moja tu tangu Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa wito wa uchunguzi huru kuhusu matukio ya utekaji na mauaji nchini Tanzania.

Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali yake haikubaliani na yanayotokea, na kifo chochote kile kinaumiza na wale wanaotaka kuonesha huruma zao wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *