
Dkt Adolf Rutayuga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET).
Na Mdoe Kiligo, MeCAP
BARAZA la Tafa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi hapa nchini (NACTVET) limesema kwamba matokeo ya uchaguzi wa awamu ya pili kwa waombaji wa Programu za Afya na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 yametangazwa Agosti 18 mwaka huu, 2024.
Katika taarifa yake kwa Umma Baraza hilo limesema kwamba lilifungua dirisha Julai 11 hadi Agosti 10 mwaka huu, 2024 ambapo jumla ya waombaji 20,163 walikamilisha maombi yao kwa kuchagua programu walizozipenda.
Aidha, NACTVET katika taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mtendaji Dkt Adolf Rutayuga imesema jumla ya waombaji 3,806 hawakuwa na sifa kwenye Programu walizoomba.
“Jumla ya waombaji 13,201 wamechaguliwa kujiunga katika vyuo 206 vinavyotoa programu mbalimbali za Afya na Sayansi Shirikishi, wanawake ni 6,512 (49.3%) na wanaume ni 6,689 (50.7%). Waombaji 193 walichaguliwa kwenye vyuo 33. vya sera na waombaji 13,008 katika vyuo 173 visivyo vya sera”, imesema sehemu ya taarifa hiyo kwa umma.
Taarifa hiyo imesema, waombaji wenye sifa ambao hawakuchaguliwa kutokana na ushindani katika programu na vyuo walivyoomba wanashauriwa kuomba kujiunga katika programu na vyuo wenye nafasi katika dirisha la awamu ya tatu kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja.
“Waombaji wote wanaweza Kuangalia matokeo ya uchaguzi kupitia tovuti ya Baraza (www.nactvet.go.tz) na kubonyeza CAS Selection 2024 kwa ajili ya kupata taarifa. Aidha, Baraza linautaarifu umma kuwa dirisha la awamu ya tatu limefunguliwa tarehe 18/08/2024 hadi tarehe 30/08/2024” imesema taarifa hiyo ya Agosti 20 mwaka huu.