
Jengo la Ofisi za Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.
Na Waandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Idara za Usafi na Usafirishaji katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam wamelalamika kwamba kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi kazini.
Katika barua ya Juni 10 mwaka huu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, wafanyakazi hao wamelalamika kwamba wamekuwa wakicheleweshewa mishahara yao, huku wakinyimwa baadhi ya posho zikiwemo za sikukuu huku watumishi wa Idara nyingine wakilipwa.
“Posho ya sikukuu baadhi ya wafanyakazi wenzetu wanapata na wengine hawapati. Sasa hatujui ubaguzi huu unatokana na nini. Na ukionekana unahoji basi unaambiwa utafukuzwa kazi, kwahiyo inasababisha usumbufu mkubwa”, imesema sehemu ya barua hiyo ambayo pia imetumwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mbunge wa Jimbo la Temeke na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo.
Wafanyakazi hao pia wamelalamikia ukosefu wa vitendea kazi vikiwemo Gloves, Gamboots, Matoroli, Refender,, Maziwa, Leki, Majembe na Max, sambamba na kima kidogo cha mishahara wakisema hautoshi na hivyo wanaomba uongezwe.
Kabla ya barua hiyo, kulikuwa na taarifa kwamba wafanyakazi wa Manispaa hiyo
Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira wamekuwa wakilalamika kwamba haajalipwa posho zao za muda wa ziada kwa zaidi ya miezi 6 sasa, na kwamba wanazo taarifa kuwa posho hizo zimetumika katika matumizi mengine kinyume cha utaratibu.
Wafanyakazi hao walimwambia mwandishi wetu kwamba wanafanya kazi katika mazingira magumu, ofisi yao haina hadhi na vitendea kazi, na wao wenyewe
hawana vitendea kazi zikiwemo Gloves, Masks, Makoti, hawapewi maziwa licha ya
kufanya kazi katika maeneo hatarishi yenye taka wakati mwingi wa kazi zikiwemo siku za sikukuu, Jumamosi na Jumapili.
Wafanyakazi hao wamemlalamikia Mkuu wa Kitengo hicho Bw. Nkana Mohammed ambaye amedaiwa kuwa amekuwa na lugha chafu na dharau kwa wafanyakazi wenzake, hataki ushauri na kwamba amekuwa kiburi kwa madai kwamba anayemsikiliza ni mtu mmoja tu kwa maana ya Mkurugenzi Mtendaji tu ambaye ndiye amemleta katika Manispaa hiyo.
“Hapa kwetu tuna malalamiko mengi. Hata kampuni inayozoa taka katika masoko yetu ya Geblasa General Supplies imepewa kazi hiyo kinyume cha utaratibu,, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu, na sheria za manunuzi”, amelalamika mmoja wa wafanyakazi wa Kitengo hicho.
“Hata kabla ya kupewa kazi hiyo, kampuni hiyo ambayo kazi yake kubwa ni kunyonya majitaka ilikuwa ikifanya kazi hiyo ya kuzoa taka, ikitumia magari ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, huku madereva wanaofanya kazi
hiyo wakilipwa posho ya shilingi 30,000 kwa kila safari moja.” amesema.
Taarifa zinasema kwamba matokeo ya kupeana kazi kirafiki, yamesababisha
kampuni hiyo kulipwa pesa nyingi ambazo hazilingani na kazi ambazo inafanya, ikitolewa mifano kwamba tarehe 24/7/2023 kampuni hiyo imeomba kulipwa shilingi 52,650,000/-; tarehe 05/02/2024 kampuni hiyo iliomba kulipwa kiasi cha shilingi 45,320,000/-; na tarehe 29/04/2024 ikiomba kulipwa shilingi 47,400,600/- zote kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kazi ya kunyonya majitaka, bila kubainisha ni maeneo gani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Elihuruma Mabelya alikanusha tuhuma hizo akisema kuwa hazina ukweli wowote huku akitishia kuchukua hatua.
“Tuhuma zote hizo sio za kweli, na kuanzia sasa nitawataarifu watendaji wa idara zote husika ili tujue hatua za kuchukua” amesema Mabelya kwa njia ya simu.