A/INSP HADINANI W.C.E.OÂ BUGURUNI
NA JONES MWANGONDA
Jeshi la Polisi Kata ya Buguruni limewataka wananchi wa maeneo hayo kushiriki kikamilifu kwenye ulinzi shirikishi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi zaidi ya 200, Inspekta wa Polisi Kata ya Buguruni, I. Hadinani, aliwaasa wananchi kushiriki bila kukosa akisisitiza kuwa hiyo ni kwa mujibu wa sheria.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kata ya Buguruni, akiwemo diwani wa kata hiyo, Busora Pazi, Kaimu Mtendaji wa Mtaa, Fadhili Kalugira na Mwishehe Bwegete Mwenyekiti wa CCM Kata ya Buguruni.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Mariam Tully Mwenyekiti wa Mtaa wa Malapa, na Said Nassoro, Mwenyekiti wa CCM tawi la Malapa.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika nje ya ofisi ya serikali ya mtaa wa Malapa, Inspekta Hadinani alitoa elimu ya ulinzi shirikishi baada ya mwenyekiti wa mtaa kusema kuwa wananchi wamegoma kulinda na kulipa ada ya ulinzi.
Katika mkutano huo ulikuwa na agenda mbili ya afya na mazingira, ulinzi na usalama, Inspekta Hadinani alisema sheria ya ulinzi wa umma ya mwaka 2022 inamtaka kila mkazi kushiriki ulinzi kwa kutoka na kulinda mtaa wake.
“Ila kutokana na utafutaji wa kiuchumi shughuli zinapishana hivyo mtu anashindwa kujipanga basi sheria imeruhusu kurudi kwenye mkutano na kupanda kiasi ambacho kwa ambaye hawezi kutoka kulinda,” alisema inspekta Hadinani.
Akisitiza kuhusu sheria hiyo Inspekta Hadinani alieleza kifungu cha 9 cha sheria hiyo, kuwa kinaeleza kuwa yeyote asiyeshiriki ulinzi shirikishi atachukuliwa hatua ambayo ni jela miezi sita au faini sh30,000 au vyote kwa pamoja.
Inpekta Hadinani alionya kwa kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu ulinzi shirikishi la sivyo atachukua hatua za kisheria.
Aidha, Inspekta Hadinani alizungumzia suala la malezi ya watoto kuwa wanajiingiza sana kwenye uhalifu kwa kufuata mkumbo hivyo wazazi, walimu na viongozi wa dini washirikiane kwa pamoja kuelimisha watoto maadili mazuri.
“Tushirikiane kwa pamoja kuwaelimisha vijana wenu dhidi ya uhalifu wanouiga katika makundi rika,” alisema inspekta Hadinani.
Alisema makundi rika huwafanya vijana kuiga vitendo vya kiuhalifu ambavyo havifai na kuacha vitendo hivyo inakuwa ngumu na kama hatua za haraka hazijachukuliwa.
Alitoa mfano wa mvuta sigara kuwa alianza ‘kugongea’ kuomba sigara kutoka kwa makundi rika matokeo yake inampa uraibu ambao anashindwa kuacha.
Inspekata Hadinani alitumia fursa hiyo kuomba sana wananchi wajikite katika malezi bora kwa watoto wao kufuatilia nyendo zao wasijiingize katika makundi mabovu.