Marehemu Lugano Ulli Mbwina

Marehemu Balozi Ferdinand Ruhinda

NA MDOE KILIGO

GIZA nene limegubika katika tasnia ya habari kufuatia vifo vya Wahariri wakongwe wawili Balozi Ferdinand Ruhinda na Lugano Mbwina waliofariki dunia katika nyakati tofauti.

Habari zinasema Balozi wa zamani wa Tanzania katika nchi za Canada na Jamhuri ya Watu wa China na Mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini, Bw. Ferdinand Kamuntu Ruhinda, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Ruhinda ambaye alipata kuwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo, na yale ya Serikali ya Daily News/Sunday News kwa nyakati tofauti, atazikwa Jumatatu, Juni 17, 2024 kwenye makaburi ya Kondo, Kunduchi, mjini Dar es Salaam.

Balozi Ruhinda ambaye pia alikuwa mwanzilishi wa magazeti ya Mwananchi na Redio Uhuru amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu akikakabiliwa na maradhi ya kisukari.

Msiba wa Mhariri huyo aliyekuwa rafiki mkubwa wa Rais wa Awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa upo nyumbani kwake, Masaki mjini Dar Es Salaam na taarifa zaidi kuhusu msiba huo itatolewa baadaye leo Jumamosi, Juni 15, 2024.

Taarifa nyingine zinasema Lugano Uli Mbwina ambaye ametumikia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya IPP Media, magazeti ya Mwananchi na The Citizen amefariki Dunia.

Mmoja wa ndugu wa karibu wa Mbwina amesema mwili wa Mhariri huyo unatarajiwa kusafirishwa kwenda mkoani Mbeya kwa mazishi.

Wakili Msomi Aloyce Komba ambaye pia ni Mwanahabari, amesema ameguswa na kifo cha Lugano kwasababu alikuwa msaada mkubwa kwake kitaaluma.

“Ni mmoja wa waandishi wa habari na wahariri wakongwe waliokuwa wanawatia moyo sana kwa sauti ya upole waandishi wa habari chipukizi nikiwemo mimi niliyeacha kazi ya ualimu wa shule za sekondari mwaka 1993 na kujiunga na TSJ kwa kujisomesha mwenyewe kwa kuandika makala katika magazeti mbambali na shughuli zingine za ujasiriamali” ameandika Wakili Msomi Komba na kuongeza:

“Bw. Mbwina alinitia moyo pia wakati nasoma sheria, na kufurahia mafanikio yangu hasa ya kuwa Wakili wa Kujitegemea”.

Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi Wahariri hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *