NAHODHA wa Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi, Jacob Massawe amesema licha ya Simba kuwa bora lakini wasitarajie mchezo mwepesi kutoka kwao kutokana na namna walivyokuwa na kiu ya matokeo mazuri kwa sasa.
Namungo ilizinduka katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC na kufanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Sasa, baada ya Simba kukubali kichapo cha aibu jana cha mabao 5-1, dhidi ya Yanga, nao Namungo wametamba kufukua mshono huo Novemba 9, mwaka huu kwenye Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumzia hilo, Massawe amesema wanatambua Simba ni timu kubwa na wanauheshimu ukubwa wao, lakini soka lina matokeo ya aina tatu, hivyo wako tayari kuhakikisha wanapambana ili kuondoka na alama tatu.
“Kila mchezaji anafahamu kucheza na Simba au Yanga ni timu za namna gani lakini ni lazima tucheze maana wote tunahitaji matokeo mazuri, na dakika 90 zitaamua,” amesema na kuongeza.
“Ligi ni ngumu sana na ina ushindani ni mkali kila timu inapambana kupata matokeo mazuri sehemu yoyote ile, unaweza kufungwa nyumbani ukashinda ugenini ndio soka,” amesema.
Katika michezo minane ambayo Namungo imecheza msimu huu imeshinda mmoja tu, ikipata sare nne na kupoteza mitatu ikiwa na alama saba, ikishika nafasi ya 12, huku Simba yenye pointi 18 ikishika nafasi ya tatu kwa mechi saba tu