Na BBC
Akizungumza siku ya Jumatatu, António Guterres alionya kwamba hali katika eneo hilo “zaidi ya mgogoro wa kibinadamu, ni mgogoro wa ubinadamu”.
“Mamia ya wasichana na wavulana wanaripotiwa kuuawa au kujeruhiwa kila siku,” Guterres aliambia mkutano wa waandishi wa habari, usiku wa kuamkia mwezi wa kwanza kamili tangu Hamas ilipoanzisha mashambulizi yake dhidi ya Israel, na jeshi la Israel likajibu kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Guterres alitoa wito tena wa kusitishwa kwa mapigano mara moja.
Matamshi yake yalikosolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen, ambaye aliandika “shame on you” kwenye mtandao wa X – ambao zamani ulijulikana kama Twitter – akiunganisha ujumbe huo na mkuu wa Umoja wa Mataifa.
“Zaidi ya watoto 30 – miongoni mwao mtoto wa miezi 9 pamoja na watoto wachanga na watoto ambao walishuhudia wazazi wao wakiuawa kikatili – wanazuiliwa kinyume na matakwa yao katika Ukanda wa Gaza,” alisema na kuongeza:
Nukuu:
“Hamas ndio tatizo la Gaza, sio hatua za Israel za kuliondoa kundi hili la kigaidi.”
Wakati mapigano yanapoingia katika wiki yake ya tano, hayaonyeshi dalili ya kupungua, huku takwimu za hivi punde kutoka wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas zikipendekeza watu 10,022 sasa wameuawa katika eneo hilo – ikiwa ni pamoja na watoto 4,104 – tangu kampeni ya Israeli kuanza.
Israel ilianza kushambulia kwa mabomu Gaza baada ya Hamas kuua zaidi ya watu 1,400 nchini Israel na kuwateka nyara wengine zaidi ya 200.
Takwimu za vifo vya Gaza zinatoka wapi?
Idadi ya vifo inayoendelea Gaza inatolewa na wizara ya afya ya eneo hilo, ambayo inasimamiwa na Hamas.
Wizara hiyo inasema kifo kinapotokea kutokana na shambulio la Israel, hospitali husajili maelezo hayo kwenye kompyuta. Maelezo yaliyowekwa ni pamoja na jina kamili, umri, nambari ya kitambulisho na jinsia.
Taarifa hizi huhamishwa kila siku kutoka kwa hospitali binafsi hadi kwenye mfumo mkuu wa kompyuta na kukusanywa na wizara. Baada ya kuchakatwa, data hutolewa kwa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina (PCBS).
PCBS iliiambia BBC kuwa takwimu hizo zinahusu wale waliofariki hospitalini pekee – haiwahusu waliouawa chini ya majengo au ambao hawawezi kutambuliwa.