Ujenzi wa ukuta unaojengwa kwenye eneo la Kanisa la Anglikana maeneo ya Buza Kwa Mama Kibonge, na kusimamiwa na wachina kama wanavyoonekna kwenye picha
Na MWANDISHI WETU
Ujenzi wa ukuta mkubwa unaojengwa kwenye eneo linalomilikiwa na kanisa la Anglikan maeneo ya Buza kwa mama Kibonge karibu na soko Temeke jijini Dar es Salaam, unafanywa kwa kukiuka sheria za kazi, ujenzi na ukwepaji wa kodi za serikali.
Morningstar POST, imebaini kuwa ujenzi huo unasimamiwa na raia wa kigeni kutoka China wanaofanya kazi kwenye kiwanda cha Colourful Industries Ltd ambacho kinahusika na kutengeneza mikeka ambao hawajasajili mradi huo kwenye mamlaka husika ikiwemo Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB), ambayo inahusika kusimamia wakandarasi wanaofanya miradi ya ujezi.
Uchunguzi wa tovuti hii umebaini kuwa raia hao wa kigeni kutoka kiwanda hicho, ambaye alikutwa katika eneo la mradi aliyefahamika kwa jina la FA HE maarufu kama Katoto alikutwa akisimamia mradi huo bila ya kuwa na kampuni ya ujenzi na hakuweka bango kwenye eneo la mradi linaloonesha makampuni yanayosimamia mradi huo, hivyo mradi huo kukwepa kulipa tozo mbalimbali zinazotokana na usajili wa mradi hivyo kupunguza pato la taifa.
Morningstar POST imebaini kuwa raia hao wa kigeni kutoka China, wanakiuka sheria kwa kutumia mgongo wa kanisa la Anglikana kufanya ujenzi kiholela na kukiuka baadhi ya sheria za nchi kwa kusimamia mradi wa ujenzi kinyume na vibali vyao vya kufanya kazi hapa nchini.
Mwandishi wa habari hizi alipofika eneo la mradi huo kupata ufafanuzi alitakiwa na Mkurugenzi wa kiwanda cha Colourful Industries Bi. FU HE maarufu kama Lina kuwasiliana na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la William Kota ambaye katika hali ya kushangaza alimtukana mwandishi wa habari hizi matusi ya nguoni akimshutumu kutaka kujua kuhusu taarifa hizi.
Hata hivyo, Morningstar POST inafanya taratibu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kiongozi huyo aliyejitambulisha kama kiongozi wa kanisa la Anglikan ambaye ofisi zake ziko maeneo ya Ilala Dar es Salaam.
Aidha, katika hatua nyingine kampuni ya Coulorful Industries imelalamikiwa pia kwa kujenga kiwanda hicho kwenye eneo la karibu na hifadhi ya bonde la mto Msimbazi kinyume na sheria za uhifadhi wa mazingira.
Wakazi wa maeneo hayo wameonesha wasiwasi wao kwa kiwanda hicho kujengwa karibu kabisa na mto kunaweza kusababisha athari kubwa hasa katika kipindi hiki kinachotarajia kuwa na mvua kubwa za Elininyo.
Ujenzi wa ukuta unaojengwa kwenye eneo la Kanisa la Anglikana maeneo ya Buza Kwa Mama Kibonge, na kusimamiwa na wachina kama wanavyoonekna kwenye picha