Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Bi Magdalena Mtenga (wa kwanza kushoto) alipokuwa akimuuliza swali Mmiliki wa mgodi mdogo wa dhahabu ulioko Ikungi mkoani Singida Bwana Ahmed Magoma (kulia) wakati ya ziara ya Ujumbe toka Ofisi ya Makamu wa Rais ilipotembelea mgodi huo

Na IBRAHIM KADILO

Mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Singida, Bw. Ahmed Magoma, amekanusha madai ya kuuza mgodi wa dhahabu ulioko Ikungi mkoani Singida.

Akizungumza na Morningstar Post, kwa njia ya simu, Bw Magoma alisema kuwa yeye bado ni mmiliki wa mgodi huo na amelipa vibali vyote vya mgodi huo hivi karibuni.

Alisema taarifa za kuuzwa kwa mgodi huo si za kweli kwa sababu ukitaka kuuza mgodi lazima kuhusisha ofisi za wizara ya madini hivyo ni suala ambalo haliwezi kufanywa kinyemelea.

Aidha alimtaka mwandishi wa habari hizi kuendelea kufanya uchunguzi wa taarifa hizo ili kupata ukweli na kuandika habari zilizothibitishwa pande zote.

Bw Magoma alijibu madai hayo baada ya taarifa iliyoandikwa na waumini wa mskiti wa Mwananyamala wakidai kuwa shekhe Idd alihusika katika kufanya udalali wa kuuza mgodi huo na kupata fedha nyingi.

Katika taarifa hiyo ambayo nakala yake Morningstar Post imefanikiwa kuipata, waumini wameingia mgogoro na shekhe wao ambaye ni imamu wa msikiti huo kuhusiana na madai ya kuuzwa kwa mgodi na shekhe kuingia mgogoro wa kifedha na madalali wengine kwenye biashara hiyo.

Morningstar Post inaendelea kufanya uchunguzi zaidi ikiwemo kutembelea mgodi huo na kuzungumza na viongozi wa  madini kwenye kanda hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *