Na Fred Okoth, Tanga
MBUNGE wa Jimbo la Handeni Vijijini, Mh. John Salu ameweka wazi kwamba ameamua kuvalia njuga kilimo cha mihogo na mkonge ili kuokoa wananchi katika jimbo lake.
Mh. John Salu akiongea na waandishi wa habari hizi jimboni kwake, alisema dhamira yake kubwa kuingia kwenye siasa ni kuendelea kutoa mchango wake katika maendeleo ya nchi yake na wananchi wa jimbo lake kwa ujumla kupitia fursa zilizopo hususan kwenye kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu.
“Hii nchi imebarikiwa sana na hizi baraka tulizopewa na Mwenyezi Mungu, tusiishie kusema tu mdomoni bali tuweke kwenye vitendo haswa kwa kuona wananchi wananufaika,
Kwa Handeni Vijijini, kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo cha mihogo na katani pamoja na mazao mengine mengi, lakini kwa sasa naweka msisitizo mkubwa kwenye mihogo na mkonge kwa sababu mbili kubwa. Mosi, mazao haya mawili yanahimili mabadiliko ya hali ya hewa vile vile kuna soko la uhakika,” Mheshimiwa Salu alifafanua.
“ Ni muhimu kuwa na mipango thabiti inayotekelezeka kabla ya kuanza kufanya kazi yeyote ya maendeleo na ni vyema kuweka mpango kazi ili iwe dira wakati wa utekelezaji. Hivyo wakulima wanatakiwa waweke malengo yao ya kilimo kwa kuangalia usalama wa chakula na kipato,” Mh. Salu anashauri.
Mh. Salu anasema harakati zake ni mipango ambayo inamsaidia mkulima kupata chakula cha kutosha na fedha ili kuondokana na umaskini.
Mh. Salu alisema zao la mihogo ni muhimu wilayani Handeni na huzalishwa karibu katika kata zote. Hata hivyo wakulima wengi bado wanatumia mbegu za asili ambazo hutoa mavuno kidogo.
Kiongozi huyo, alisema kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine, jitihada zinafanywa za kusisitiza matumizi ya mbegu za kisasa za mihogo.
Akizungumzia zaidi zao la mihogo alisema faida za zao la mihogo ni kwamba hustahimili ukame.
Aidha, akizungumzia zao la mkonge alisema kuwa kwa sasa anataka kuimarisha zao la mkonge kwa kuhamasisha wakulima wadogo na wakubwa kwa kuwa zao hilo ni la kibiashara linafaida kubwa kwa wakulima.
Akaongeza kuwa katika jimbo lake vikundi mbalimbali vya wakulima vimekwishaanza kulima zao hilo la mkonge na yeye kama mbunge wao yuko tayari kuunga mkono wakulima wote wa zao hilo hata kwa kuanzia kilimo cha heka mbili.
“Mimi nimeenda Brazil ambako wakulima wakule hata wale wadogo wadogo wanalima zao la mkonge……..tofauti na huku kwetu ilizoeleka kuwa wakulima wakubwa ndio wakulima mkonge…..tunataka kubadilisha fikra hizi kwa hapa kwetu hata wakulima wadogo walime mkonge kwa faida yao”, alisema.
MBUNGE wa Jimbo la Handeni Vijijini, Mh. John Salu