Kamanda Mchunguzi aomba wazazi wapeleke watoto kanisani na msikitini

Na Jones Mwang’onda, Tanga

Jeshi la Polisi jiji la Tanga limefanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kiasi kikubwa kwa kuwakamata baadhi ya vijana waliokuwa wanafanya uvunjaji na uporaji wa mali za wananchi.

Akizungumza na Morningstar POST ofisini kwake Chumbageni Tanga, Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga,  Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Almachius Mchunguzi, alisema kuwa makundi ya vijana waliokuwa wanafanya uhalifu katika maeneo mbalimbali hasa eneo la Duga wamedhibitiwa.

“Naomba wazazi kwa dini zao, yaani wakristo wawapeleke watoto Sunday School na waislamu wawapeleke madrasa kujifunza maadili ya dini zao……wakiwa na hofu ya Mungu, watakuwa waadilifu hata kwenye ajira na maisha yao kwa ujumla”, alisema Kamanda Mchunguzi.

Kamanda Mchunguzi ambaye  hapendezwi sana na makundi ya vijana wahalifu kuitwa majina kama watoto wa ibilisi kwani  wao ni wahalifu kama wahalifu wengine.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo Tanga katika kudhibiti uhalifu ni pamoja na kuwakamata na baadhi yao kufikishwa mahakamani na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhalifu.

Alisema, jeshi la polisi Tanga limefanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kushirikiana na wananchi na vikundi vya ulinzi shirikishi.

Hata hivyo, kamanda Mchunguzi amesema wanajiandaa kutoa mafunzo kwa vikundi hivyo namna ya kufanya kazi kwa weledi ili wasiwe kero kwa wananchi  bali wawe msaada kwao.

Kamanda Mchunguzi alisema kuwa Jeshi la polisi lilizindua kampeni ya kupunguza uhalifu nchini kwa kuongea na wazazi kupitia kampeni inayojulikana kwa kauli mbiu ya “ongea nae”.

Kampeni hiyo ambayo inasimamiwa na Mtandao wa Polisi Wanawake kwa Tanga ilizinduliwa Korogwe.

Alisema mtandao  huo utasaidia kupunguza uhalifu kwa kutoa elimu kwa wazazi kwa kuongea na watoto wao maadili mema ya malezi wakiwa wadogo.

Akizungumzia kuhusu madawa ya kulevya aina ya mirungi, Kamanda Mchunguzi, alisema kuwa Tanga wamedhibiti uhalifu huo licha ya kuwa changamoto kubwa ni madawa hayo kupitishwa kutoka nchi ya jirani ya ambayo imehalalisha madawa hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *