Na Ibrahim Kadilo na Fred Okoth
Kampuni ya Wilmar Tanzania Limited ambayo inazalisha mafuta ya kupikia ya Korie ambayo gazeti hili la mtandao ilitoa taarifa zake za unyanyasaji wa wafanyakazi wametishia kwenda mahakamani iwapo habari zao hizitofutwa mtandaoni.
Tishio hilo la kwenda mahakamani limeifikia Morningstar Post kupitia kampuni ya mawakili itwayo LA LEGIS ATTORNEYS na kusainiwa na wakili, Hance Mrindoko, huku ikiwasilishwa kupitia njia ya e-mail na whatsapp.
Katika ‘Demand Notice’ hiyo, wakili msomi Mrindoko anaeleeza kwamba gazeti hili la mtandao halikutoa nafasi ya mlalamikiwa kujieleza, na hiyo ni habari ya kashfa kwa mteja wao (defamatory article) wakati waandishi wa habari hizo walifanya kikao na wasemaji wa kampuni ya Wilmar katika ofisi zao zilizopo Barabara ya Nyerere, maeneo ya Vinguguti baada ya barua mbili za maswali, ambazo zote kampuni hiyo inakiri kupokea.
Morningstar Post inabaki na msimamu wake kwamba habari hii haina kasoro na wapo tayari kwenda kortini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kuwa sauti ya wasio kuwa na sauti.
Katika habari ya awali, Wilmar Tanzania inatuhumiwa kunyanyasa wafanyakazi wake na kukiuka taratibu za ajira kwa wafanyakazi.
Akijibu tuhuma hizo mwanasheria wa kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa inafahamika kwa jina la Murzah Oil, Bi. Lulu Kissambu alikanusha tuhuma hizo na kutetea kampuni hiyo kuwa inafuata taratibu zote za ajira kwa wafanyakazi wake.
Bi Kissambu alikiri kuwa Seif Ismail Makala na Hamisi Hamza Mbogo walikuwa ni wafanyakazi wao wakiwa kama madereva na walikuwa na mikataba ya ajira tangu mwaka 2016 na kampuni hiyo.
Bi Kissambu hakutaka kutoa maelezo ya kina, alisema kwa kufupi kampuni yake ina uhakika kuwa wamefuata taratibu zote za sheria ya ajira katika kuwafukuza kazi wafanyakazi hao.
Akijibu tuhuma za madai hayo kuwa mfanyakazi wao Hamis Mbogo alikuwa hawasilishiwi michango yake ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kipindi cha nyuma akiwa ameajiriwa na kampuni ya Murzah, alisema kuwa kampuni yake inaongoza kwa kuwa kampuni kubwa inayowasilisha michango ya wafanyakazi NSSF.
Licha ya wafanyakazi hao kufukuzwa kazi bila barua notisi, barua ya kusitisha mkataba wa ajira, bila kupewa haki ya kusikilizwa na kuona barua ya kufukuzwa kazi, na kushtakiwa polisi kwa kuhusishwa na wizi, Mwanasheria wa kampuni hiyo alisema kuwa huo sio unyanyasaji wa wafanyakazi.
Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu (HR), Emmanuel Christopher akizungumzia tuhuma hizo alisema kazi ya kushtaki kwa makosa ya jinai ni ya polisi wao kama kampuni hawapaswi kuulizwa kuhusu suala la wafanyakazi wao kupelekwa polisi kwa tuhuma za wizi.
Wakizungumza na Morningstar POST, wafanyakazi wa kampuni hiyo Seif Makala na Hamisi Mbogo walisema kuwa wamenyanyaswa na kufukuzwa kazi bila kufuata taratibu za ajira.
Walisema kuwa walituhumiwa kuiba trela la gari lenye thamani ya sh35/m na kupelekwa polisi lakini polisi wameshindwa kuendelea na kesi hiyo baada ya kuona kuwa hawahusiki katika wizi huo.
Alisema kuwa mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu Bw Emmanuel na Lyamuya waliwaandikia barua ya kuwafukuza kazi bila kuwapa nafasi ya kuisoma barua hiyo na kuona yaliomo badala yake waliwataka kusaini bila kupata nakala wala kusoma barua hiyo.
Walisema kuwa hatua hiyo ya kutakiwa kusaini barua bila kujua kilichoandikwa walikataa, hivyo mpaka wanashindwa kupata haki zao za michango yao iliyopo NSSF.
Walisema kuwa kitendo cha kuwabambikikizia kesi kilifanywa na watu wa idara ya rasilimali watu kwa chuki binafsi lakini hakuna sababu ya msingi ya kufukuzwa kazi.
Wafanyakazi hao wamemuomba meneja wa kampuni hiyo Bw. Mathew kufuatilia kwa makini suala hilo kwa kuwa linafanywa na watu wa idara ya rasilimali watu ambao wanachuki binafsi na baadhi ya wafanyakazi.
Taarifa zaidi kuhusu Sakata hili zinaendelea katika machapisho yajayo.
Ofisi za kampuni ya Wilmar Tanzania zilizoko barabara ya Nyerere maeneo ya Vingunguti jijini Dar es Salaam