Dar es salaam
Maisha ni fumbo, huwezi kujua nini kitatokea kesho, kama wanachokipitia Mzee Hashim Msuya na mkewe, Lilian Kunda kinasadifu fumbo hilo. Ni kipindi ambacho wazee hao wenye miaka zaidi ya 80, walikuwa wametulia, wanakula matunda ya watoto wao.
Bila shaka kuna siku mzee Hashim na mkewe Lilian, walilala njaa kuhakikisha vijana wao wanasoma kwa lengo la kuwaandalia kesho nzuri ili baadaye waanze kuwatunza wakiwa wazee.
Katikati ya matunda ya watoto wao wanne waliokuwa wakiendelea kuvuna, ghafla ajali ya barabarani inakatisha maisha ya watoto wao.
Mama atoa ya moyoni kupoteza wanaye wanne ajalini
Kauli ya mwisho ya Sia kabla kufariki
Hussein Mtiro, ambaye ni mdogo wa mzee huyo jana aliiambia Mwananchi kuwa: “Wamebaki kama walivyoanza.”
Watoto hao wanandoa hao, walifikwa na mauti usiku wa kuamkia jana saa 6:11 katika ajali ya gari aina ya Toyota Prado na Scania, katika Kijiji cha Mapatano, Kata ya Mbwewe, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Gari hiyo iliyokuwa na wanandugu wa familia moja, waliofariki dunia papo hapo ni, Neechi (48), Daina, Dk Norah na Sia.
Neechi alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Majanga wa Benki ya ABSA ambaye alizaliwa Desemba 24, 1974, Norah alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tawi la Dar es Salaam, Diana alikuwa mfanyabiashara huku Sia akifanya kazi Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ilala jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo akizungumzia ajali hiyo alisema gari hiyo ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kilimanjaro, ikiendeshwa na Neechi Msuya, huku Scania ilikuwa ikitokea Arusha ikiendeshwa na Philipo Mtisi.
Kamanda Lutumo alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Prado kuhama kutoka upande wa kushoto wa barabara kwenda kulia kisha kogongana uso kwa uso na lori hilo.
Alisema miili ya wanadugu hao ilihifadhiwa Zahanati ya Lugoba kwa uchunguzi wa daktari kisha ilisafirishwa hadi Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam na kupokewa na ndugu, jamaa na marafiki.
Mtiro, ambaye ni ndugu wa baba wa marehemu hao, akizungumza na gazeti hili kuhusu taratibu za mazishi alisema, “zitajulikana leo baada ya kikao kufanyia, hasa kujua Sia, Diana na Dk Norah watazikwa wapi, kwani walikwisha olewa; waume zao wameomba wakawasiliane kwanza na ndugu zao na kesho (leo) tutafanya kikao cha pamoja sasa.”
Alisema kama itakuwa vinginevyo watafanya shughuli ya pamoja ya kuwaaga kwenye uwanja mmoja, huku akisema msiba kwa hapa Dar es Salaam utakuwa Mbezi Beach, nyumbani kwa Dk Norah. Mtiro alisema marehemu wote wameacha watoto.
Mmoja wa ndugu wa wanafamilia ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema, ndugu zao hao walikuwa wanakwenda Kilimanjaro kwenye mazishi ya mdogo wao upande wa baba yao mdogo na mazishi yalikuwa yafanyike jana mchana.
“Mara ya mwisho tulikuwa nao jana (juzi) wanachangisha michango ya kumsafirisha ndugu yetu (kutoka Dar es Salaam alipofikwa na mauti) na wao kutokana na majukumu yao, hawakwenda na mwili, waliamua kumaliza kazi zao kwanza na wakaondoka jioni ili wafike usiku na washiriki mazishi, lakini ndicho kilitokea.”
Awali, katika nyumba hiyo Mwananchi ilimkuta mtoto mwenye umri kati ya miaka kumi hivi ambaye alisema mzee Msuya na mkewe waliondoka jana kwenda katika msiba.
“Waliondoka jana mchana wamekwenda katika msiba,” alisema mtoto huyo, akichota maji kwenye bomba lililoko nje ya nyumba hiyo.
Majirani wa familia iliyopoteza watoto wote wanne katika ajali ya gari, wameomba wanaume waliooa mabinti wa mzee Msuya wakubali wazikwe mahali pamoja.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Uzunguni jijini Dodoma, Kamishna Msaidizi mstaafu wa Jeshi la Polisi, Kassim Muhija alisema kwa kufanya hivyo kutamwezesha baba wa mabinti hao kushiriki mazishi ya wanawe wote.
“Mimi ningeomba hao wanaume watatu waliooa kwa mzee Msuya wakubali watoto hawa wazikwe mahali pamoja kwa sababu mzee hawezi kujigawa, maana mmoja kaolewa Musoma mwingine Kilimanjaro na mwingine sijui Mwanza,” alisema Muhija, ambaye ni rafiki wa karibu wa mzee Msuya.
Hata hivyo, Muhija jana kwa siku nzima alikuwa akimpigia simu ya mkononi ya mzee Msuya bila mafanikio.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Salimin, Uzunguni jijini Dodoma, Edna Ndejembi ambaye alicheza na ndugu hao wakati wa utoto wao, alisema msiba huo ni pigo kwa mtaa huo.
“Sisi wa mtaa huu tuna taratibu zetu kwamba mwenzetu akipatwa na msiba tunashirikiana. Pamoja na kwenda kumfariji na kumwezesha kihali na mali. Naomba wanamtaa tuendelee kudumisha utaratibu wetu wa kufarijiana japokuwa wenzetu hawapo hapa,” alisema.
…Mzumbe, Benki ya Absa
Chuo Kikuu cha Mzumbe wakimzungumzia Norah, walisema marehemu alikuwa mhadhiri wao katika kampasi ya Dar es Salaam kwa miaka 12 akifundisha masomo ya sheria na utawala.
Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu, alisema marehemu alihamia hapo tangu Mei 2011 akiwa ametokea katika kitivo cha sheria kampasi kuu ya Morogoro na kuwa naye hapo kwa takribani miaka 12.
Profesa Binamungu alisema Norah alikuwa akifundisha masomo ya sheria katika programu mbalimbali za biashara pamoja na utawala.
“Kimsingi Norah katika utumishi wake alikuwa ni nguzo sana katika kubeba mzigo wowote ule kwenye programu zetu zote zinazohusu masuala ya sheria,” alisema Profesa Binamungu.
Alisema Norah amefariki akiwa katika ngazi ya mhadhiri mwandamizi katika idara ya masomo ya utawala.
Profesa Binamungu alisema moja ya mambo watakayomkumbuka katika majukumu yake hapo chuoni, alikuwa kiungo katika kampasi yao, mbali ya kuwa mhadhiri pia alikuwa ni katibu wa kampasi hiyo na alidumu kama mkuu wa idara kwa muda mrefu.
“Kiukweli wanafunzi wake pia watam-miss sana katika ushauri wake, alikuwa ni mbobezi katika kuangalia ni jinsi gani tamaduni zetu zinavyosimama kama kigingi kwa maendeleo ya kina mama.
“Norah alikuwa amebobea zaidi katika hilo akichunguza tamaduni zetu ambazo ni potofu zimesimama kama vikwazo cha utekelezaji wa kuondokana na ubaguzi kati ya kinamama na kinababa, alijikita kwenye hilo na ilikuwa ndio centre yake,” alisema Profesa Binamungu.
Rafiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Mary, alisema amesoma na Norah kuanzia shule ya awali hadi sekondari na katika kipindi chote alimjua marehemu kama mtu anayependa kujichanganya na watu na mkarimu kwa kila mtu.
Kwa upande wa Benki ya Absa kupitia Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Beda Buswalo alisema ni kweli Neechi Msuya alikuwa mfanyakazi wao na ni mmoja kati ya viongozi wa ngazi ya juu ya benki hiyo, akiwa anaripoti moja kwa moja kwa mkurugenzi mtendaji.
Buswalo alisema Neechi alikuwa akihudumu katika benki hiyo katika nafasi ya Ofisa Mkuu, akishughulikia majanga na hatari zozote zinazoweza kuiathiri benki.
“Msuya (Neechi) hapa kwetu ndio alikuwa msimamizi wa hicho kitengo cha kuangalia majanga yoyote yatakayoikumba benki na kuhakikisha kuwa yanadhibitiwa ili yasiweze kuiathiri benki,” alisema.
Pia, alisema marehemu alijiunga na benki yao tangu Novemba 2021 katika nafasi hiyo na amefariki akiwa katika wadhifa huohuo. “Kiukweli tumeguswa na kifo chake, hakuwa tu mfanyakazi mwenzetu, bali alikuwa katika safu ya uongozi mkuu wa benki,” alisema Buswalo.
Alisema kwa sasa wanaendelea kuwasiliana na familia na kusaidiana katika shughuli mbalimbali za kuweza kumpumzisha. Janine Mallya ambaye ni rafiki wa karibu wa Sia alisema wamekuwa wote katika kikundi cha kikoba na Juni mwishoni mwaka huu, waliandaa pamoja shughuli ya mtoto wa rafiki yao, “alikuwa anavalishwa pete ya uchumba na siku hiyo, yeye (Sia) alisimamia suala zima la sala.”
“Mara ya mwisho nimeongea naye Alhamisi ya wiki iliyopita, tena ilikuwa asubuhi anauliza vikao vitaanza lini siku zinakwenda. Sasa ameondoka hata harusi hatashiriki tena,” alisema Janine.
Wengine waliotoa salamu zao za rambirambi katika msiba huo ni mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo, ambaye alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo kwa kuwa wote walikuwa bado katika umri wa kutegemewa sana na jamii. “Walikuwa wasomi na wajasiriamali wazuri, lakini kubwa zaidi walikuwa wapenda maendeleo na waliokumbuka na kujali nyumbani kwao Msangeni, Ugweno.
“Naiombea familia pamoja na wote walioguswa na msiba huu, faraja, amani na utulivu tunapoelekea kwenye taratibu za kuwapumzisha wenzetu hawa,” alisema, alipozungumza na Mwananchi kuhusu msiba huo.
