NA WAANDISHI WETU
MAISHA ya Fidel Castro Ochieng, 19, mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Olembo sasa yananing’inia kwenye mwamba, huku madaktari wakijizatiti kuondoa risasi tisa mwilini mwake alizomiminiwa na polisi wakati wa maandamano ya wiki hii Kisumu.
Ochieng’ ni miongoni mwa mamia ya waathiriwa wa ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji katika sehemu tofauti za nchi mnamo Jumatano.
Muuguzi mkuu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) Bi Teresa Okiri alisema mnamo Ijumaa kwamba, mvulana huyo aliletwa humo akiwa na risasi nane kifuani mwake na nyingine kwenye mkono wake wa kulia.
“Tunamtayarisha ili afanyiwe upasuaji kuondoa risasi hizo kutoka mwilini mwake,” akasema Bi Okiri.
Wakati wa mahojiano kitandani mwake, Ochieng’ alielezea kwamba, alikuwa akicheza karata na marafiki zake kwenye veranda ya nyumba yao katika mtaa wa Nyamasaria, kundi la maafisa wa polisi walipowavamia.
Kingine anachokumbuka ni maafisa wakipiga mayowe kwamba wamewapata, baada ya kuwasaka kwa muda mrefu.
“Mmoja wao aliwaambia wenzake kwamba, tulikuwa tumejificha baada ya kuzua fujo na ndipo wakaanza kutucharaza kwa marungu,” akasema Ochieng’.
Vijana hao walipojaribu kutoroka, polisi mmoja alichomoa bastola yake na kuwafyatulia risasi kadha wakiwa mbioni. Ochieng’ alimiminiwa risasi nane akikimbia ili kujinusuru.
Alibahatika kupata msamaria mwema aliyemsaidia kumtorosha kwa pikipiki yake. Lakini walipokuwa wakitoroka, afisa huyo alifyatua risasi nyingine iliyomjeruhi Ochieng’ mkononi.
Mvulana huyo anasema ni bahati kwamba yungali hai kwa sababu afisa huyo wa polisi aliendelea kuwafuata huku akifyatua risasi hadi walipoingia kwenye lango la hospitali ya JOOTRH.
“Nahisi uchungu zaidi, sijaweza kulala kutokana na mwasho wa risasi zilizoko kifuani mwangu,” akasema Ochieng’ alipokuwa akisafirishwa kwa machela kupelekwa katika chumba cha upasuaji.
Akaongeza, “mmoja wa marafiki zangu alikufa kutokana na majeraha ya risasi alipokuwa akipokea matibabu. Nashukuru Mungu kwamba ningali hai,” akasema Ochieng’.
Jana Ijumaa, muuguzi Okiri alithibitisha kuwa wagonjwa wawili ambao pia walikuwa na risasi kadhaa mwilini mwao walifanyiwa upasuaji na wanaendelea kuhudumiwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji huduma maalumu (HDU).
Alisema wengi wa wahasiriwa walioletwa katika hospitali hiyo ni vijana wa kiume wenye risasi zilizokwama vifuani, migongoni au mikononi mwao.
“Kwa ujumla, watu 20 waliletwa hospitalini humu jana wakiwa na majeraha ya risasi. 15 waliokuwa na risasi mwilini walifanyiwa upasuaji na risasi hizo kuondolewa,” akasema Bi Okiri.
Miongoni mwao ni Joseph Odhiambo, 22, ambaye ni mhudumu wa bodaboda, Collins Ochieng, 20, Tonny Owigo 21 (mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Great Lakes) na Calary Ochieng, 19, waliofanyiwa upasuaji kuondoa risasi mgongoni, miguuni na viunoni.
Bi Okiri alisema watu wawili walikufa hospitalini humo Alhamisi na hivyo kufikisha sita, idadi ya waliokufa kutokana na majeraha ya risasi au kipigo cha polisi wakati wa maandamano.
Siku hiyo, mwanamume mmoja kwa jina Dave Aghan alikufa mjini Bondo baada ya kuripotiwa kupigwa risasi na polisi.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay, Lameck Owuor, 28, ambaye ni mkazi wa Rongo, kaunti ya Migori, anapokea matibabu baada ya kupigwa risasi shingoni Jumatano wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Wengine waliolazwa katika hospitali hiyo wakiwa na majeraha ya risasi ni Derrick Otieno, 18, aliyefanya mtihani wa KCSE mwaka jana. Kwa ujumla, hospitali kubwa katika eneo zima la Nyanza zimelemewa na idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa kwenye makabiliano na polisi katika maandamano hayo yaliyoanza Jumatano.
Wakazi wanasema wengi wao walishambuliwa kwa risasi na polisi ilhali wengine walipatwa na risasi kimakosa wakati wa makabiliano hayo.
Katika kaunti ya Nakuru, naibu msimamizi mkuu wa hospitali ya Nakuru Level Five Dkt Samuel Wanjara jana alithibitisha kifo cha mgonjwa mwingine miongoni mwa wale waliojeruhiwa wakati wa maandamano mjini Nakuru.
Mtu mwingine alikufa Jumatano baada ya kupigwa risasi na polisi wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na polisi mtaani Shabaab Jumatano. Shirika la Amnesty International linasema jumla ya watu 30 wameuawa na polisi kwenye maandamano tangu Machi 2023.
