Na Happyness Hans, WAF – ARUSHA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Emmanuel Nchimbi amewataka viongozi na wakuu wa Idara wanaowazuia waandishi waendesha Ofisi kushiriki mikutano ya chama hicho kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Amesema hayo leo Mei 21, 2026 Mkoani Arusha kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 13 wa Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA), unaoambatana na uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho.
“Tunatamani kila kiongozi awapende, awajali, awape safari, motisha na kuwapongeza pale wanapofanya vizuri,” amesema Dkt. Nchimbi.
Mhe. Dkt. Nchimbi amesema Ofisi yoyote bila uwepo wa waandishi waendesha Ofisi ni sawa na gari lisilo na usukani, kwani wao ndiyo sura na lango la Ofisi. Amesema hakuna mtu anayeweza kuonana moja kwa moja na kiongozi bila kupitia kwa mwendesha Ofisi.
Aidha amesema waandishi waendesha Ofisi wamekuwa msaada mkubwa katika Taasisi mbalimbali na kwa sasa ni sehemu ya kufanya maamuzi pamoja na kupanga mikakati ya maendeleo ya Ofisi.
“Ninyi waandishi waendesha Ofisi mnajua mambo mengi kuliko wengine, hivyo mnapaswa kuwa msaada kwa watu wengine, ninyi ni watu muhimu sana Ofisini,” amesema Nchimbi.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa TAPSEA unaotarajiwa kufanyika Mei 22, 2026, Dkt.Nchimbi amewapongeza viongozi wanaomaliza muda wao kwa mchango mkubwa walioutoa katika kuimarisha taasisi hiyo na kuifikisha katika hatua nzuri.
Pia amewataka viongozi hao kusimamia uchaguzi huo kwa haki na uwazi ili kuhakikisha wagombea na wapiga kura wanapata haki zao bila vikwazo.
“Tunawashukuru viongozi wote kwa kazi nzuri mliyoifanya na kuifikisha taasisi katika hatua nzuri. Nawaagiza kusimamia vizuri uchaguzi, mkizingatia haki na uwazi. Kwepeni vitendo vyovyote vya kukwamisha haki za wagombea na wapiga kura,” amesema Dkt. Nchimbi.