NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Wilaya ya Temeke, imemuhukumu Sajidu Omary Salum kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kuiba fedha kiasi cha Shilingi za Kitanzania 177,456,645.30.
Hukumu ya shauri hilo la jinai namba 000032017/2024, ilitolewa Disemba 22, 2025 na hakimu Mkazi Frank Lukosi, ambapo Mshtakiwa Sajidu alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuiba akiwa mtumishi (Stealing by Servant) kinyume na Kifungu cha 258 (1) na 271 cha Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022).
Inaelezwa kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2022 na Agosti 2023, katika eneo la Sokota, lililopo Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa ni mfanyakazi wa Africa Energy Limited, aliiba kiasi hicho cha fedha.
Aidha, ilielezwa ripoti ya mwisho ya ukaguzi wa hesabu ilithibitisha upotevu wa fedha, ambapo zilikuwa mikononi mwake kutokana na majukumu yake ya kusimamia mauzo, kukusanya mapato na kuwasilisha ripoti, hivyo ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) ulitosha kuthibitisha kosa.
Awali, kabla ya hukumu hiyo Sajidu Omary Salum alikana shtaka na kusema; hakutendewa haki wakati wa kufukuzwa kazi na amesingizwa wizi wa fedha, kwani Mfumo wa M-Pesa haukuwa chini ya udhibiti wake, pia hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa yeye kuhusika na wizi huo.
Hata hivyo, baadhi ya wanafamilia wa mshtakiwa waliozungumza na Morning StarPost walisema, hawajaridhishwa na hukumu hiyo, hivyo wanakusudia kuwasilisha rufaa ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria na taarifa zaidi zitatolewa kupitia mtandao huu.