WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU NCHEMBA

Na Anania Njonjo

KAMPUNI ya China Enterprises Trading Limited iliyopo Kitalu namba 107, Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, inadaiwa kukiuka taratibu mbalimbali za ujenzi na ukwepaji mkubwa wa kodi.

Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na raia kutoka China, ipo kwenye hatua za ujenzi wa jengo la ghorofa tatu, nyuma ya jengo lao lasasa, huku ikielezwa kuna zuio kutoka kwa Mamlaka ya Mipango Miji, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, kampuni hiyo inadaiwa ilizuiwa kujenga jengo hilo hadi watakapobadilisha ramani yao kutoka ghorofa tatu hadi mbili ambazo zinaruhusiwa kutokana na eneo husika.

Mmoja wa maafisa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwasababu sio msemaji, alisema eneo linalozunguka uwanja wa ndege, hairuhusiwi kujenga jengo linalozidi ghrofa mbili, hivyo wahusika walizuiwa kuendelea na ujenzi huo.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu umebaini kuwa, wamiliki wa kampuni hiyo wamekahidi agizo la mipango miji la kusimamisha ujenzi, na badala yake wanaendelea kujenga kwa kutumia ramani yao ya awali ya ghorofa tatu, huku ikidaiwa wanawatumia mafundi wa kawaida badala ya kutoa tenda kwa kampuni inayotambuliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Aidha, taarifa zilizopo zinadai kwamba, kampuni hiyo inatekeleza ujenzi huo bila kuusajili Bodi ya Wahandisi (ERB) Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi AQRB.

Mbali na tuhuma hizo, inaelezwa kwenye mradi huo kuna ukwepaji mkubwa wa kodi ambapo wahusika hawajaingia mikataba na wakandarasi wanaotambulika hivyo wanaikosesha Serikali mapato, pia hawana mikataba na wafanyakazi, hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi hao ambao hawajasajiliwa WCF (Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi), NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) na OSHA (Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi).

“Ndugu waandishi niwaeleze tu, hapa hakuna ukaguzi wowote wa ujenzi uliofanyika ndio maana mapungufu yote hayajajulikana, kwa kifupi kabisa ujenzi huu unafanyika kienyeji mno na mabosi hawajali maslahi ya wafanyakazi wala usalama wao wanapokuwa kazini,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye jina lake tunalo.

Alipotafutwa Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Sami, ingawa baada ya uchunguzi kupitia namba yake ya simu ya mkononi ambayo tunayo, ilionekana imesajiliwa kwa jina la Christa Mkalawa, alishindwa kutoa ushirikiano wowote kwa ajili ya kupata ukweli wa tuhuma zilizotajwa.

Aidha, katika hatua nyingine waandishi walibaini kuwa, Afisa Uhusiano huyo amepotosha kwenye mambo mengi kwa lengo la kuficha ukweli, ikiwemo kuwaelekeza waandishi kuzungumza na Kampuni ya Midea ambayo alidai ndio wamiliki wa jengo hilo, jambo ambalo limebainika halina ukweli.

Hata hivyo, jitihada za kuendelea kufuatilia suala hilo zinaendelea ikiwemo kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ikiwemo Idara ya Mipango Miji ya jiji la Dar es Salaam kwa ajili kujua hatua ambazo zitachukuliwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu unaofanywa na kampuni hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *