Na Mwandishi Wetu

WATOTO wa Marehemu Abdallah Magonda, wakazi wa Kongowe, Wilayani Temeke, Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuingilia kati madai ya fidia kufuatia eneo lao kujengwa ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Toangoma na choo cha kulipia.

Akizungumza na MorningStarpost mmoja wa wanafamilia Jumanne Abdallah Magonda alisema, mchakato wa kudai fidia ulianza wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke akiwa Iddi Nyundo na Meya akiwa Bwanausi Kingori.

Alisema, mazungumzo baina ya Serikali, Manispaa na familia yao yalikuwa na mwelekeo mzuri, lakini yalikwama baada ya Mkurugenzi Nyundo kufariki dunia na Meya Bwanausi alipoamua kwenda kugombea ubunge wa Jimbo la Lulindi, Mkoani Mtwara.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo nakala zake tunazo, Abdallah Magonda Oktoba 20, 2006 alimuandikia barua Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kuhusu madai yake ya eneo analomiliki kuingiliwa na kujengwa ofisi hiyo, ambapo kabla ya hapo aliwasilisha barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa Agosti 1, 2005.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya niliwasiliana na Manispaa kwa barua ya tarehe 01/08/2005, baada ya kufuatilia majibu nikapata jibu la mdomo kwamba, jibu nitapata kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Toangoma. Nimesubiri mpaka sasa sijapata jibu,” inasomeka barua hiyo ya Abdallah Magonda kwenda kwa Mkuu wa Wilaya.

Barua hiyo iliendelea: “baada ya hapo niliandika demand notice ya tarehe 27/07/2006 bila majibu. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, kwa Mamlaka uliyopewa kwa waraka wa Serikali EA183/284/2001 wa Februari 2006, nakuomba uingilie kati ili nipate haki yangu ambayo ipo wazi,”

Hata hivyo, licha ya jitihada hizo za Mzee Magonda, hakufanikiwa kupata haki yake hadi umauti ulipomfika, huku watoto wake nao kwa muda mrefu wakiendelea kupigania haki yao bila mafanikio.

“Lengo letu au ombi letu, tunachohitaji ni fidia kamili kulingana na hali ya sasa, maana hii ni nchi yetu na jengo lililojengwa ni la Serikali yetu, ingawa Serikali yetu ya Manispaa ya Temeke imeingilia na kusimika jengo, tunaomba tupate kifuta machozi katika eneo hilo,” alisema Jumanne Magonda.

Alisema, kama alivyofanya baba yao, nao wameandika barua sehemu mbalimbali kuomba msaada bila mafanikio, hivyo wamemuomba Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa kuingilia kati suala lao ili walipwe fidia.

“Pia (Waziri) tunakuomba ufanye uchunguzi wa kina katika utambuzi na kujiridhisha kama kweli eneo hili ni mali ya familia ya Magonda na baada ya hapo utakuwa umeshafahamu ukweli na ndipo tutaweza kufidiwa kulingana na eneo husika,” alisema Jumanne.

Aliendelea kusema: “Mwisho kabisa chonde sisi wanafamilia ya Magonda, tunakuomba Waziri wetu kupitia Serikali yetu sikivu ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, mtufidie ili tuweze kujikwamua na hali zetu duni.”

Mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kuwapata viongozi wa Serikali kwa ngazi ya Kata na Wilaya kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, hata hivyo jitihada zaidi zinaendelea ili kuhakikisha familia hiyo inapata haki yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *