Na Ripota Wetu
SHULE ya msingi na awali ya Nice future iliyopo kwa Robert, Kata ya Mbezi Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam imefanya mahafali kwa ajili ya kuwaaga wanafunzi wanaotarajia kumaliza darasa la Saba na Shule ya Awali.
Mahafali hayo ya tano na ya kwanza kwa darasa la saba toka kuanzishwa kwa shule hiyo, yalifanyika Agosti 22, 2025 kwenye ukumbi wa Little flowers uliopo maeneo ya Mazulu, barabara ya Goba, ambapo yalipambwa na maonyesho ya mitindo ya mavazi na sarakasi ambayo yote yalifanywa na wanafunzi wa madarasa tofauti walioandaliwa na waalimu wa shule hiyo.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bwana Delphine Magoto aliwashukuru wazazi wote kwa mchango mkubwa waliotoa katika kufanikisha sherehe hizo na pia aliwashukuru wakuu wa shule jirani ikiwemo Rungwe na Shule ya Msingi Mbezi na nyinginezo kwa ushiriki wao.
“Kitaaluma shule ya Nicefuture iko vizuri na inategemea wanafunzi wote kufaulu vizuri tayari kwa kuanza sekondari, pia shule yetu ina waandaa watoto wetu katika maadili mema na kumcha mungu kwa dini tofauti,” alisema Magoto.
Kwa upande wake, Dkt. Elikana Manyirizu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, aliwashukuru viongozi wote na waalimu kwa kazi nzuri ya kufanya mageuzi ya elimu katika shule hiyo.
Alisema, kutokana na jitihada zinazofanywa na walimu hao, kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto, huku wakiendelea na uboreshaji wa mazingira ya shule hiyo ikiwemo kujenga madarasa na ofisi za walimu licha ya changamoto ya wazazi kuchelewa kulipa ada za watoto wao.
Aidha, Dkt. Manyirizu alitumia nafasi hiyo kuwasihi wazazi kulipa ada kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya shule hiyo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya upatikanaji wa elimu.