Na Mwandishi Wetu
Chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha azimio la kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Azimio hilo limepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia chama hicho. Chama hicho pia kimempitisha Dkt. Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar.
Uamuzi huo umefanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake. Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara) ambapo mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira alipitishwa kushika wadhifa huo jana Jumamosi.