NA MWANDISHI WETU
Chama tawala nchini Tanzania (CCM), kimeitaka wizara yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa (Tamisemi), kupuuza makosa madogo madogo katika ujazaji wa fomu ili kuruhusu wagombea wengi zaidi kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na wanahabari hii leo, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt Emmanuel John Nchimbi amesema: “…natumia fursa hii kutoa wito kwa Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa, tunatambua kuwa wamefuata sheria, lakini tunaomba katika hatua ya mwisho ya rufaa kupuuza makosa madogo madogo ili Watanzania wengi wapate kugombea,” amesema Nchimbi.
Dk. Nchimbi alipoulizwa kuhusu madai ya uwepo wa undumakuwili wa kuruhusu wagombea wa CCM wanaojaza fomu kimakosa na kuwaondoa wagombea wa upinzani, wanaofanya makosa sawa na hayo, amesema “undumilakuwili wa aina yote haukubaliki na huo ndio msimamo wa CCM.”
Tamisemi yatoa tamko
Akizungumza leo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa, (TAMISEMI), amesema suala la kuenguliwa sio la upendeleo bali ni utekelezaji wa kanuni kwani hata wagombea wa CCM wanaenguliwa.
Waziri huyo amevionyooshea kidole cha lawama baadhi ya vyama vya upinzani akisema vinafanya propaganda kwa kusambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii huku wagombea wao wakiwa nyumbani badala ya kufuata utaratibu wa kukata rufaa kama kanuni zinavyotaka.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unaosimamiwa na TAMISEMI, unatarajiwa kufanyika nchi nzima tarehe 27 Novemba mwaka huu, ambapo Watanzania watapata fursa ya kuwachagua Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Mchanganyiko) na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake).