
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
SERIKALI imeahidi kufikisha mawasiliano kwenye maeneo yote yenye idadi kubwa ya watu na maeneo yote ya pembezoni, kwa kujenga minara ya simu ili kuondoa tatizo la mawasiliano hasa kwa njia ya simu.
Ahadi hiyo imetolewa tarehe 6 Juni, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), wakati akijibu maswali ya baadhi ya Wabunge waliotaka kufahamu mipango ya Serikali katika kumaliza tatizo la mawasiliano ya simu.
Miongoni mwa Wabunge hao ni Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemus Maganga, aliyetaka kufahamu ni lini minara ya simu itajengwa ili kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, yenye kata 17 zikiwemo Mbogwe, Nanda, Nghomolwa na Lulembela, pamoja na maeneo mengine ya uchimbaji.
Akijibu swali hilo, Mhandisi Maryprisca amesema, Serikali itakwenda kufanya tathmini kwenye maeneo hayo na maeneo mengine nchini yenye mahitaji makubwa ya mawasiliano, ili kufahamu mahitaji halisi.
Kwa upande wa Mbunge wa Mwibara, Mwita Waitara aliyeiomba Serikali kuweka minara ya simu kwani wananchi wa jimbo hilo wanasikiliza redio na kuangalia TV za Kenya, Naibu Waziri huyo amesema, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unafanya tathmini kwenye maeneo ya mipakani ikiwemo maeneo ya Jimbo la Mwibara, ili kuweka minara.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Abeid Ighondo Ramadhani, Mhandisi Maryprisca amesema, UCSAF imeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya TTCL ili kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ngingu Kijiji cha Mlamba, Kata ya Msisi vijiji vya Mnung’una na Mkwawe, na Kata ya Msange vijiji vya Mringa na Endesh.
Amesema, UCSAF pia imeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya Vodacom ili kufikisha huduma za mawasiliano katika Katika cha Msinko kata ya Ugandi, na kwa Kijiji cha Migugu Kata ya Mudida, UCSAF imeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya Halotel.