Na Mdoe Kiligo, MeCAP


KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET), Dkt. Adolf Rutayuga, Aprili 2 Aprili mwaka huu amekutana na ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Ujumbe huo uliongozwa  na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi) wa Chuo hicho Kikuu cha Zanzibar, Dkt. Ali M. Ussi na Afisa Sheria Mwandamizi wa SUZA, Ndg. Mtaib A. Othman, katika ofisi za NACTVET Kanda ya Mashariki, Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Ugeni huo umetembelea Baraza kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya urekebu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Miongoni mwa waliohudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya NACTVET.
Taarifa ya NACTVET imesema kwamba ujio wa ujumbe wa SUZA unafuatia maelekezo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kuangalia namna bora ya kurejesha vyuo vya kati vilivyounganishwa chini yake 2016.
“Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo cha Utawala wa Fedha Zanzibar (ZIFA); Chuo cha Sayansi ya Afya (CHS); Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar (ZIToD); na Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kizimbani” imesema taraifa ya NACTVET.

Baraza hilo lenye dhamana ya kusimamia elimu ya ufundi na mafunzo stadi hapa nchini limesema kwenye taarifa hiyo kwamba mchakato wa utekelezaji huo  unafanyiwa upembuzi kwa ushauri elekezi wa Kamati ya Ufundi, iliyoundwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa ushirikiano wa karibu na SUZA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *