
Marehemu Gilbert Lyimo, ambaye ndugu zake wanalalamika kwamba malipo ya fidia ya bima kutokana na kifo chake yamekuwa ni utata bado.
KAMPUNI ya Bima ya Insurance Group of Tanzania (IGT) imelalamikiwa na baadhi ya wateja wake kwa kutowalipa malipo ya fidia ya bima kwa wakati.
Mmoja wa walalamikaji hao ambaye amezungumza na mtandao huu amesema kwa miezi kadhaa amekuwa akifuatilia malipo ya bima ya ndugu yake ambaye alifariki kutokana na ajali ya basi la Dar Express mwaka 2021.
Mlalamikaji ni Lameck Lyimo ambaye anadai kwamba ndugu yake Gilbert Lyimo alifariki kwa ajili ya basi hilo namba T 155 BEU ambayo iliyotokea katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Jijini Dar es Salaam.
Lameck amesema pamoja na kufuata taratibu zote za kudai malipo ya fidia katika kampuni hiyo lakini kumekuwa na ugumu wa kulipwa malipo hayo kiasi kwamba familia nzima ya marehemu imekuwa na maswali kuhusu uwezo wa kampuni hiyo ya Bima.
“Kuna wakati wanasema kwamba watatulipa kidogo kidogo, sidhani kama kuna utaratibu wa aina hiyo katika kufidiwa pale kunapokuwa na tatizo. Nadhani mamlaka husika zinatakiwa kuangalia uwezo wa kampuni hizi, lakini kuyabeba na kuyatatua malalamiko ya wananchi” amesema.
Mtandao huu umekuwa ukifuatilia ukweli wa malalamiko haya, lakini kumekuwa na ugumu wa kuwapata wahusika, hata hivyo jitihada za kupata ukweli na majibu ya msingi kutoka Mamlaka zenye dhamana ya kusimamia shughuli za bima zinafanyika.