Mwenyekiti wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mercy Sila akizungumzia tuzo za wanawake wajasiriamali zinazotarajiwa kutolewa na taasisi hiyo Machi 16, 2024. Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Afrika Elibariki Shammy na Mkurugenzi wa TWCC Mwajuma Hamza
Na Mwandishi Wetu
Tuzo za wanawake wajasiliamlia zinazotarajiwa kutolewa na taasisi ya Wanawake Wafanyabiashara nchini TWCC, ni fursa kwa wanawake wajasiliamali nchini.
Mabilioni ya fedha yanatarajiwa kutolewa kuwawezesha wanawake wa kitanzania wenye kujitoa na kufanya shughuli za ujasilimali kuweza kupata mafunzo na kuwezeshwa kifanyabiashara.
Uzoefu unaonesha kuwa wanawake wakiwezeshwa wanaweza hivyo taasisi hiyo ambayo imejipanga kuwawezesha wanawake wajasiliamali inapaswa kupongezwa kwa kuunga mkono wanawake wajasiliamali nchini.
Fursa hii sasa inapaswa kuchangamkiwa na wanawake hapa nchini ili kujikwamua na ule wimbo kuwa hatuna mtaji wa kufanya biashara badala yake kujidhatiti na kulenga kujikwamua kiuchumi.
Katika kujipanga kuwezesha kundi kubwa la wanawake taasis ya Trade Mark Afrika Elibariki imetenga bilioni 4 kuwawezesha wanawake wajasilimali zitakazotumika kwa miaka minne kwa mafunzo na kuwapatia fursa za kufanyabiashara
Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Africa, Elibariki Shammy amesema utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa wanawake wanaofanya vizuri kwenye biashara ili kutoa hamasa kwa wengine ili waongeze juhudi.
Shammy amesema wanawake wafanyabiashara wanapitia changamoto nyingi zinazowafanya wengi wao wakate tamaa au kushindwa kukuza mitaji yao, hivyo uwepo wa miradi inayowajengea uwezo na kuwapa motisha wanaofanya vizuri ni hatua ya muhimu.
“Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wanawake wafanyabiashara kuanzia kwenye mazingira yenyewe ya biashara, masuala ya kifamilia, kukosa kuaminiwa kwenye taasisi za fedha zinazotoa mikopo na mambo mengine mengi.
“Ndiyo maana mradi huu upo na tangu umeanza tunaanza kuona mabadiliko, angalau baadhi ya wanawake wamekuza biashara zao kutoka hatua moja kwenda nyingine, ili kuwapa hamasa wengine ni lazima hawa wapewe motisha ikiwamo hizi tuzo zinazoenda kutolewa na TWCC katika kusherehekea mafanikio ya wanawake,” amesema Shammy.
Akizungumzia tuzo hizo zitakazotolewa Machi 16, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema zitahusisha vipengele 20 kutoka kwenye sekta mbalimbali ikiwamo ya kilimo, uzalishaji, madini, usafirishaji, biashara nje ya nchi, mawasiliano, usimamizi wa hafla, mama lishe, ufugaji na ufungashaji.
Vipengele vingine ni ujenzi, afya, elimu, utalii, uhandisi, biashara za kuvuka mipaka, sanaa na teknolojia ya habari.
Amesema tuzo hazitatolewa kwa watu kupigiwa kura bali kuomba au kupendekezwa na watu wengine watakaovutiwa na kazi za wahusika kisha timu ya chemba hiyo itapitia maombi na mapendekezo hayo kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa.
Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni uendelevu wa biashara, kiasi cha mtaji kisichopungua Sh5 milioni, nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wafanyabiashara wanaohusika na uzalishaji, umiliki wa biashara na waliojikita kwenye kilimo biashara.
“Nitumie fursa hii kuwaita wanawake wajasiriamali kujitokeza kuomba kutuma maombi au kama kuna mwanamke unaona anastahili unaweza kumpendekeza sisi tutafuatilia kuhakikisha amekidhi vigezo vyetu na kama anastahili basi atakuwa miongoni mwa tutakaowatambua,” amesema Mwajuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila amesema jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali zinaongeza hamasa ya wanawake kuingia kwenye biashara na kujitengenezea kipato.
“Tunaona Serikali inafungua nchi na kuboresha mazingira ya uwekezaji, wanawake wanaendelea kuchangamkia fursa hii na kufanya biashara ingawa bado biashara nyingi ni zile ndogo ndogo na ukweli ni kwamba wanawake wanaogopa kukua kwa kuhofia changamoto watakazokutana nazo mbele endapo watakuza biashara zao,” amesema Mercy