Na Prince Junior
Utafiti wa kina unaonesha kuwa, miongoni mwa sababu za ndoa nyingi kuvunjika miaka ya karibuni ni wanaume ‘kufulia’ maisha kuishiwa kipato .
Kwa mujibu wa uchunguzi, kundi kubwa la wanawake miaka ya sasa hupenda kuolewa na wanaume wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na inapotokea mume ametetereka, pesa imekimbia, mke huanza visa na kukimbia.
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wanandoa waliyowahi kufarakana ambapo wanaume wengi walidai kuachwa baada ya kutetereka kiuchumi.
“Nilipomua mke wangu mwaka 2017 nilikuwa vizuri sana kiuchumi. Nilikuwa na kampuni ya kulisha taasisi moja kubwa nchini.
“Kwa hiyo pesa ilikuwepo kwa kadiri ya uhitaji wowote nyumbani. Magari ya kutembelea yalikuwepo mawili. Mbali na gari la kusambazia bidhaa kwenye taasisi.
“Bahati mbaya sana uongozi ulibadilka. Kwa hiyo tenda pia zikafa. Hali ikaanza kuwa mbaya. Ilifika mahali nikauza magari moja baada ya jingine hadi yote yakaisha.
“Ndipo nipoanza kuona upande wa pili wa mke wangu. Alianza visa, kukosa adabu, kujibu anavyotaka mwishowe akasema eti mimi nimebadilika tabia. Akaondoka,” alisema Hamis Mzee, mkazi wa Mwenge, Dar.
Shabani John, mkazi wa Buza anasema kuwa, mkewe aliyezaa naye watoto wawili alimkimbia siku tatu tu baada ya yeye kufukuzwa kazi kwenye kiwanda kimoja cha kutengeneza vifaa vya plastiki licha ya kwamba waliishi miaka sita.
“Yaani siku hiyo narudi nyumbani namwambia nimefukuzwa kazi. Tukakaa siku ya kwanza, ya pili, ya tatu huyoo kwao.
“Tena nilitoka, nilikwenda Temeke kwa rafiki yangu. Narudi nakuta kachukua kila chake. Sikumfuata kwa sababu hakuchukua kilicho changu.
“Kwa hiyo kama unasema nitoe maoni, yangu ni hayo. Siku tatu bila kazi, mke kashindwa kuishi na mimi kama alivyoishi miaka sita nikiwa na kazi,” anasema Shabani.
Kipimo cha mahojiano kinaonesha lawama za wanaume wengi zinafanana kwamba, kufulia kwao kumekuwa chanzo cha ndoa kuvunjika na wake kukimbiwa.
Wanaume wengi wamesema kwamba, ishara kuwa ndoa zao kuvunjika chanzo ni kuishipa pesa, wake zao wakishaondoka huwa hawarudi kwa wazazi wao bali huenda kupanga na kuishi maisha mazuri
Hali hiyo hutafsiriwa na wanaume kuwa, wakiwa ndani ya ndoa wenza wao hao walikuwa wadangaji na ndiyo sababu ya kutaka kuishi wenyewe.
Hata hivyo, wanawake nao kwa upande wao wamekuwa wakijitetea kwamba, ndoa zao siku hizi zinavunjika sana kwa sababu wanaume wanakwepa majukumu.
‘Mimi ni mke wake. Sasa pesa ya kusuka haipatikani kwa wakati kama ilivyo kwa wanawake wenzangu, wao wanapendeza tu maana waume zao wanawajali.
“Nikikuomba pesa ya saluni leo huna. Kesho huna. Unadhani nini kitatokea? Ndoa itavunjika tu, nikatafute maisha mengine na wanaume wengine,” anasema Betha Mathew, mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumzia kadhia hiyo, Mchungaji Lawrence Mchaka wa Kanisa la Kipentekoste lililopo Duga jijini Tanga, alisema kinachowatatiza wanandoa wengi wa zama hizi ni kusahau viapo vyao wakati wa kufunga ndoa madhabahuni.
“Inakuta mtu na akili zake timamu kabisa anasema, ‘naahidi nitakuwa nawe katika raha na shida,’ watu wanapigia magofi tamko hilo.
“Lakini mambo yakiharibika kwenye ndoa, mwenza wake kaishiwa au mwenza wake hazai, anataka kuachana.
“Mimi nawaomba watu wanaotaka kuingia kwenye ndoa wajitafakari kwanza maana vile viapo vina maana kubwa sana,” alisema mchungaji huyo.