NA MWANDISHI WETU
YANGA inajiandaa kuvaana na Al Ahly ya Misri katika mechi ya pili ya hatua ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL),lakini kocha wa Wananchi hao Muargentina, Miguel Angel Gamondi,ameusoma mchezo mzima wa maandalizi kwa timu zote mbili akatamka kwa ujasiri kwamba Waarabu hao wamekwisha.
Gamondi amesema Yanga inajua uchungu wa kufungwa na Al Ahly mara kwa mara lakini safari hii anataka kuandika historia mpya.Yanga inazo sababu kuu tano muhimu ambazo zinaipa jeuri timu hiyo na kuwafanya mashabiki wake kujiuliza Al Ahly wanatokaje?
Chini ya kocha Hans Van Pluijm, Yanga mwaka 2014 ilivunja mwiko wa kutozifunga timu za Kaskazini mwa Afrika,baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya hao Al Ahly.Shukrani kwake mfungaji wa bao hilo pekee nahodha, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ Uwanja wa Benjamin Mkapa (zamani Taifa), Dar es Salaam na kwa mara ya kwanza, Yanga ikashangilia ushindi dhidi ya Ahly, timu ya Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla.
Hata hivyo, katika mchezo wa marudiano raundi ya kwanza mjini Alexandria, Misri, wenyeji Ahly walilipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, hivyo mchezo ukahamia kwenye dakika za nyongeza na baadaye penalti ambako ilitolewa kwa penalti 4-3.
Mara ya mwisho Yanga na Al Ahly kukutana ilikuwa mwaka 2016, Wananchi wakatolewa kwa jumla ya mabao 3-2, wakitoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, kisha wakaenda kufungwa 2-1, Cairo nchini Misri.
Wanajangwani hao sasa watakutana tena na Al Ahly Desemba 2, mwaka huuDimba la Mkapa, hiyo sasa ikiwa ni hatua ya makundi na si mtoano tena.
Lakini, Gamondi amesema kwamba, ni lazima Yanga washinde kwa idadi kubwa ya mabao katika mechi hiyo kwani ushindi katika mchezo huo unabeba matumaini makubwa ya kutimiza malengo yao msimu huu.
“Tunataka kuanza hesabu hapa nyumbani, tunahitaji kushinda kwa gharama yoyote, Al Ahly ni timu kubwa na tunaiheshimu na tunaifahamu lakini kama tuna nia ya kufika robo fainali ni lazima tushinde nyumbani upate pointi tisa.
“Kwetu haijalishi watafunga bao ama la, kama watafunga sisi tufunge zaidi, siwezi kusema mangapi, hayo yatafahamika uwanjani, ninawafahamu vizuri tangu nikiwa katika mataifa kule ya Kiarabu na hata hapa Yanga hivyo ninajua nitakavyokwenda kucheza nao kwani kikosi changu cha sasa kimeimarika,” alisema Gamondi.
Kauli hiyo ya Gamondi inasadifu msemo uliopo kwamba; historia zipo kwa ajili ya kuvunjwa tu kwani hata katika klabu kubwa za soka za Ulaya historia nyingine za miaka hata 50 iliyopita ndio zinavunjwa leo ama mwaka huu, hivyo huo unaweza kuwa mwanzo wa historia mpya ya Yanga.
Al Ahly ndiyo timu inayoshikilia rekodi ya kutwaa taji la michuano hiyo mara nyingi zaidi ikiwa imefanya hivyo mara 11 katika miaka ya 1982, 1987, 2001, 2005, 2006, 2008, 2012, 2013, 2020, 2021 na 2023 inakutana na Yanga ikiwa bingwa mtetezi wa kombe hilo, huku viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Marcel Koller, wakionyesha hofu kubwa mbele ya Wanananchi.
Hofu yao kubwa inatokana na matokeo ya mwaka 2014 waliponusurika kutolewa na Wanajangwani hao, hivyo kuwafanya Al Ahly kuiweka Yanga kwenye kundi la timu ngumu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.Yafuatayo ni mambo matano yatakoifanya Yanga iwastajabishe Al Ahly