NA MWANDISHI WETU
KAMA kuna nyakati ngumu ambazo Simba inapitia ni sasa. Ni muda ambao umoja katika timu unahitajika kwa kiwango kikubwa sana.
Ni rahisi tu kusema kwamba Wekundu hao wa Msimbazi wana hali ngumu, kuanzia katika uongozi, benchi la ufundi, wachezaji hadi kwa wanachama na mashabiki kwa ujumla hali ni tete.
Kwa sasa tunaweza kusema ndio mashabiki wasiokuwa na furaha zaidi katika ardhi ya Mama Samia Suluhu Hassan. Kuna watu tangu wafungwe 5-1 na Yanga wamekimbia miji yao kukimbia kelele za Wananchi.
Lakini ukiangalia haya yanayoendelea ni ya kujitakia na wala hakuna kupepesa macho, lazima ukweli usemwe ili viongozi wajitafakari.
Kuna maswali mengi yanaelekezwa kwa uongozi, tangu tu usajili wa dirisha kubwa msimu huu walivyokuwa wanaufanya. Unajiuliza kama Mwekezaji, Mohamed Dewji ‘MO’ alitoa Bilioni 3 za usajili ndio kuleta wachezaji wa daraja la chini kiasi hiki?
Unajiuliza Bilioni 3 zimesajili wachezaji gani? Inaelezwa MO Dewji aliongezea tu fungu la usajili lililotengwa kwa msimu huu, sasa klabu imetoa kiasi gani cha fedha ya usajili?
Achana na hilo, waza kuhusu yule skauti aliyetambulishwa, Mels Daalder raia wa Uholanzi ambaye tulielezwa kwamba atasaka wachezaji kwa ajili ya kuja kuitumikia Simba. Jíulize yuko wapi? Ameleta wachezaji gani?
Lakini chini ya kapeti, inaelezwa kwamba yule skauti alifanya kazi yake kwa ufasaha tu, na kuna wachezaji aliwatafuta waje Msimbazi, ila uongozi wakawapiga chini. Fikiria hapo.
Kama alipeleka majina ya wachezaji kama Yao Kouassi, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli ili waje kuongeza nguvu katika kikosi cha Simba. Yule jamaa alikuwa msaada mkubwa na anajicho la kiufundi.
Ila, inasemekana kwamba kuna Wanasimba wasioitakia mema klabu yao wakawasogeza Yanga na leo ndio chachu ya ushindi katika kikosi chao. Akili za wapi hizi?
Hapa inaonesha kabisa katika uongozi wa Simba wa sasa, sio salama kabisa, hawana nia njema na klabu yao kwa ujumla.
Si hao tu, inaelezwa skauti alipeleka majina ya wachezaji wa daraja la juu tu, lakini ndio hivyo wenye nyadhifa wakaona waizike ripoti yake.
Mbali na hivyo, ripoti yake inaonyesha ilikata baadhi ya mastaa ambao umri umeenda kama John Bocco, Saido Ntibazonkiza na Shomari Kapombe ambaye alitaka akatwe ama acheze kiungo kutokana na kupungua makali yake.
Pia, Mholanzi yule aliwatonya Simba kuwa hata Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aachwe kipindi kilekile baada ya kuisha tu kwa msimu uliopita.
Ukiangalia kile ambacho alishauri ndio kinatokea sasa. Inamaana wangebeba ripoti yake na kuifanyia kazi isingefikia hapa tulipo.
Na hata Aishi Manula alitaka atafutiwe kipa mwingine na akatafuta kipa wa Afrika Magharibi. Lakini wao wakatafuta wachezaji wa daraja la chini ndio haya yanatokea.
Lakini inaelezwa kwamba wapo viongozi ambao wanauza siri za Simba kupeleka kwa viongozi wa Yanga tena wanalipwa. Huu ni usaliti wa kiwango cha juu kwa zama hizi.
Kama wahujumu Simba watu hawa wapo ni wa kutimua tu. Tajiri MO Dewji anajitahidi sana kuwekeza na kutoa pesa zake, lakini anaangushwa na wachache.
Na viongozi ndio wanamfanya atukanwe mitandaoni kwamba hatoi pesa wakati sio kweli, na shida ipo kwa waliokalia viti pale Msimbazi.
Kuna muda namfikiria Barbara Gonzalez ambaye alikuwa anagombana nao hawa viongozi kila siku. Na ndio maana walimuundia zengwe kila uchwao.
Ukweli usemwe tu, MO Dewji anamkosa mtu sahihi wa kumsaidia ndani ya Simba ambaye atafanya kazi zake kwa usahihi kama ilivyokuwa kipindi cha Barbara.
Angalia pale Yanga leo, inaonekana ipo sahihi kwa kila kitu kutokana na GSM kupata kiongozi makini ndani ya klabu yao ambaye Injinia Hersi Said.
Hivyo hata kwa Simba, wanahitaji mtu mwenye kujitoa kama Injinia Hersi wa kumsaidia MO Dewji. Na ikiwezekana arudi tu Barbara. Maana leo kila Mwanasimba anamkumbuka huyu mwanamke shupavu.
