Na MWANDISHI WETU
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amesema kikosi chao kipo fiti kuwavaa Niger, katika mchezo wa kwanza wa Kundi E wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Katika kundi hilo, Tanzania imepangwa na Morocco, Congo Brazaville, Zambia na Niger.
Taifa Stars itatupa karata yake ya kwanza dhidi ya Niger Jumamosi hii ya Novemba 18, katika Uwanja wa Marrakech, Morocco.
Katika mchezo huo, Tanzania inahitaji pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya Jumanne (Novemba 21) kuikaribisha Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Msuva amesema kuwa, kikosi chao kinaendelea na mazoezi na kila mchezaji yupo fiti kuipeperusha bendera ya taifa.
Nyota huyo anayekipiga JS Kabylie ya Algeria, amesema wachezaji wote wanatambua umuhimu wa mchezo huo, lengo lao ni kuvuna alama tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri.
Msuva amekiri kuwa wapinzani wao wana timu nzuri yenye wachezaji bora, lakini Taifa Stars itafuata maelekezo ya benchi la ufundi na kuongeza juhudi zao binafsi kupata ushindi.
“Mara ya mwisho tulipocheza dhidi ya Niger tulishinda bao 1-0, tunakwenda kwao kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu.
“Tumejiandaa kuhakikisha tunaipambania nchi yetu, kuitwa timu ya taifa ni kupewa heshima hivyo ni lazima kujituma, tunatambua umuhimu wa kupata ushindi katika mchezo huu,” amesema.
Nyota huyo amesema matokeo mazuri watakayopata katika mchezo huo, yatawapa matumaini ya kufanya vyema zaidi katika michezo mingine.
Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, zinatarajiwa kufanyika katika nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico
