Na MWANDISHI WETU
BAADA ya Yanga kubandika bango kubwa linaloonyesha mabao 5-1, ambazo walishinda dhidi ya Simba, sasa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi wamekerwa na kitendo hicho na kugeuka mbogo kwa hasira..
Yanga leo asubuhi wamebandika mabango matatu katika sehemu mbalimbali za barabara ya Ali Hassan Mwinyi, jijini Dar es Salaam na kuzua gumzo nchini na nje ya nchi.
Lakini kubwa zaidi ni mapovu ya mashabiki wa Simba ambao wamekerwa na kitendo hicho cha Wananch kufanya hivyo, hali inayowafanya kufika mbali kuwashawishi viongozi wao kushitaki.
“Hata kama ni utani hapa Yanga imezidi, hawawezi kutumia ‘logo’ ya klabu yetu ya Simba kubandika bango lile barabarani, lazima viongozi walichukulie hatua jambo hili kwa maslahi mapana ya klabu yetu,” aliandika Abdallah Jumanne katika ukurasa wake wa Instagram.
Wakati Johnson Amos aliandika; “Watu wanafanya utani sana, ila huu ambao wanaofanya viongozi wa Yanga hapana, uongozi wangu wa Simba walibebe hili kwa kufuata mkondo wa sheria kwa maslahi mapana ya timu yetu.”
Lakini gazeti limekuwa likifuatilia ‘comments’ za katika kurasa za Yanga, baada ya kuposti bando hilo, mashabiki wa Simba wamekuwa wakali kwa kutoa hadi lugha chafu.
