Na MWANDISHI WETU

SI mchezo! Ndivyo, inavyofaa kueleza mshahara wa Sh. Milioni 25 atakaolipwa mshambuliaji wa Kaizer Chiefs, Ranga Chivaviro endapo ataamua kutua Yanga.

Yanga imekuwa ikitaka kumsajili Chivaviro tangua dirisha kubwa la usajili lililopita kutokea Marumo Gallants, lakini Kaizer Chiefs waliwazidi kete Wananchi. Sasa, taarifa zinaeleza kuwa miamba hiyo ya Tanzania imemrejea tena, na endapo watakubaliana, mshahara wake utakuwa Sh. 25,000,000 kwa mwezi.

Habari zilizopatikana wiki hii zilieleza wawakilishi wa Chivaviro, Kaizer Chiefs na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, walikutana kujadili uhamisho wa mshambuliaji huyo raia wa Afrika Kusini.

Moja ya mitandao ya Afrika Kusini, ilieleza kuwa mabosi wa klabu hiyo ya mitaa ya Jangwani, walikutana na wawakilishi wa Chivaviro, ambaye mkataba wake utakuwa wa thamani ya Milioni 400 kutua Yanga.

Lakini mbali na Yanga kutaka kufanya kufuru hiyo, ila inaelezwa itampatia nyumba ya kifahari Mbezi Beach, huku kigogo mmoja akimpatia gari ya kifahari akiwa Tanzania.

Yanga inasemekana kuvutiwa na habari kuwa Chivaviro mwenye umri wa miaka 30 anafikiria maisha mapya mbali ya Kaizer Chiefs msimu huu, baada ya kukosa namba ya kudumu katika kikosi hicho.

Chivaviro, bado ana miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa na klabu hiyo, lakini Yanga imeamua kuuvunja ili aje kuvaa uzi wa kijani ama njano au mweusi Jangwani msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *