Na MWANDISHI WETU

NYOTA wa zamani wa klabu ya TP Mazembe ya nchini DR Congo ambaye kwa sasa amerudi Tanzania kuichezea klabu ya Singida Big Stars, Thomas Ulimwengu, amesema wachezaji wengi wa kigeni wanaosajiliwa kucheza Ligi Kuu Tanzania (NBC), wanafuata malipo mazuri na umaarufu.

Akizungumza kupitia mahojiano maalum ya klabu hiyo,  Ulimwengu ambaye ni mchezaji mzawa ametolea mfano kwa nchi ya DR Congo ambako amecheza na kuishi kwa miaka mingi, amedai huko hakuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya michezo ukilinganisha na Tanzania ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangia kukuza majina ya wachezaji.

“Mimi naona wachezaji wengi wamefanya (Tanzania) kama ni njia. Wanaona kabisa nikija Tanzania nikifunga magoli kadhaa naondoka.” amenukuliwa Ulimwengu.

Sababu nyingine ametaja ni maslahi makubwa ambayo klabu za Tanzania vinatoa kwa wachezaji wa kigeni na hivyo kupelekea wachezaji wengi kuvutiwa kuja kucheza nchini.

“Klabu za Tanzania zinathamini sana wachezaji wa nje kuliko wazawa. Wanakuja hapa, wanathaminiwa sana wanalipwa vizuri. So hakuna mchezaji ambaye hapendi kwenda kwenye mpira akalipwa vizuri, wanakuja kwa sababu wanaona kuna mafanikio,” amefunguka Ulimwengu ambaye ni rafiki wa karibu na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta.

Ulimwengu ametoa wito kwa timu za Tanzania kuthamini wachezaji wazawa kwa sababu wapo wachezaji wenye uwezo mzuri na vipaji vikubwa kuliko baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *