Na MWANDISHI WETU
ZIKISALIA siku 12 tu kabla ya kukutana na Yanga katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), Kocha wa CR Belouizdad, Marcos Paqueta ameingiwa na ubaridi kwa kuona Wananchi ndio timu tishio zaidi kwenye kundi lao.
Miamba hiyo ya soka la Algeria, imepangwa Kundi D hatua yamakundi ya michuano hiyo, pamoja na Al Ahly ya Misri, Medeama SC ya Ghana na Yanga.
Paqueta raia wa Brazil kama anaweweseka hivi kuhusu Yanga, baada ya kuweka wazi mapema kuwa mchezo wao utakuwa mgumu dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania.
Akizungumza jijini Algers, alisema: “Ratiba haijakuwa rafiki kwetu ukitazama hapo mbeleni utaona kuwa tuna michezo mingi migumu mbele yetu lakini bado tumecheza mechi mfululizo.
“Tunakwenda kucheza michezo mingine mbeleni kisha ndio tutakwenda kucheza wa kwanza na Yanga ambayo ni moja ya timu ngumu Afrika, huo utakuwa ni mchezo wa kimataifa hivyo tulitakiwa kupata muda mwingi wa kujiandaa ili tuweze kufanya vizuri,” alisema kocha huyo.
Ratiba inaonyesha CR Belouizdad kabla ya kukutana na Yanga wanatarajiwa kucheza michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Paradou FC na JS Kabylie.
Baada ya hapo waje kucheza mchezo wao dhidi ya Yanga, Novemba 24 , mwaka huu nchini Algeria.
